Zachuana kusaka mshindi wa pili, zinakutana Jumapili
Dar es Salaam. Kama ni ngoma, basi bado ni mbichi kwa Azam na Simba katika harakati zao za kuwania mshindi wa pili msimu huu.
Ushindi wa mabao 4-0 na 3-0 ambao timu hizo
zilipata jana dhidi ya wapinzani wao, Stand United ya Shinyanga na
Ndanda ya Mtwara umezidisha zaidi vita hiyo ya kuwania nafasi ya pili.
Pia, ushindi huo umeifanya mechi ijayo baina ya
timu hizo mbili, Jumapili, Mei 3 iwe kama fainali, kwani ndiyo inayoweza
kuamua nafasi hiyo itakwenda kwa nani.
Hata hivyo, Azam iliyofikisha pointi 45 dhidi ya
Simba yenye pointi 41, ina mchezo pungufu ikilinganishwa na Simba, kitu
pekee kinachoipa faida zaidi katika harakati zake za kusaka nafasi hiyo.
Katika mchezo wa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, Simba ilianza kuhesabu bao lake la kwanza, mapema dakika ya
nane kupitia kwa kiungo Jonas Mkude.
Bao hilo lilifuatiwa na mashambulizi makali kwenye
lango la Ndanda, yaliyosababisha makosa dhidi ya Emmanuel Okwi na
kusababisha penalti iliyopigwa na Ibrahim Ajibu aliyepaisha na baadaye
Ramadhan Singano, Said Ndemla kupachika mengine mawili.
Ndanda ambao wako katika hatari ya kushuka daraja
walishindwa kuhimili kasi ya washambuliaji wa Simba na hivyo mabeki wao
kujichanganya kila mara wakati mwingine kumchanganya kipa wao, Salehe
Malande aliyeonekana akiwafokea kila mara.
Simba walikwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao
3-0, lakini waliporudi kipindi cha pili walishindwa kufurukuta mbele ya
Ndanda waliowabana vilivyo wasipate bao zaidi.
Nako kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam
walijipatia mabao kupitia kwa Gaudence Mwaikimba (mawili), Brian Majwega
na Farid Malick, yaliyotosha kuwapa pointi tatu muhimu mabingwa hao
watetezi.
Kwenye Uwanja wa Sokoine ,wenyeji Mbeya City
waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar,mabao
yaliyofungwa na Rafael Alpha kwa penalti, dakika ya 45 baada ya kipa wa
Kagera, Agatony Anthony kumfanyia madhambi Cosmas Fred wakati akielekea
kufunga. Bao la pili la Mbeya City, liliwekwa kimiani dakika ya 56 na
Deus Kaseke.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 52,
inajiandaa kutwaa ubingwa kesho, Jumatatu dhidi ya Polisi Morogoro
ikishinda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Imeandikwa na Charles Abel na Oliver Albert(Dar), Godfrey Kahango, Mbeya
No comments:
Post a Comment