Saturday, 2 May 2015

AGRA, serikali kukuza kilimo cha kibiashara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma
   Wasaini mkataba mpya wa kuboresha ushirikiano
Serikali imesaini mkataba mpya na Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika (Agra) unaoelenga kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara, hivyo kuleta faida zaidi na kuinua hali za wakulima wadogo nchini.
Mkataba huo ulisaini jijini Dar es Salaam juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma na Rais wa AGRA, Dk Agnes Kalibata.
Makubalino yanayofikiwa katika mkataba huo yanaweka mazingira ya kushirikiana katika kazi kati ya Tanzania na AGRA na kuainisha namna jitihada hizo zitakavyotekelezwa.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo, Kaduma alisema makubalinao hayo yatachochea ongezeko kubwa la usalama wa chakula na kukifanya kilimo kuwa chenye faida zaidi kwa wakulima wadogo.
“AGRA imekuwa mshirika wa dhati kuisaidia Tanzania katika kuleta maendeleo ya kilimo. Makubaliano tuliyoyasaini kati yetu yataufanya ushirikiano wetu katika hatua mpya,” alisema. Kwa mujibu wa Kaduma, AGRA imekuwa ikitoa mchango muhimu kwa sekta ya kilimo nchini kwa nyakati tofauti.
Miongoni mwa misaada ya AGRA katika sekta hiyo ni ufadhili kwa mpango wa kilimo kwanza unaolenga kuongeza upatikanaji wa mazao tofauti, kuwajengea uwezo washirika tofauti wa maendeleo ya sekta ya kilimo wakiwamo kampuni za mbegu, mawakala wa kilimo.
Hivi karibuni, AGRA ambayo imewekeza kiasi cha takribani Dola milioni 48 za Marekani kwa miradi yake hapa nchini tangu mwaka 2007, walizindua teknolijia mpya ya kuhifadhi mazao ikianzia na mavuno ya msimu wa mwaka 2014. 
Serikali imekifanya kilimo kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa nchi, na kutoa rasilimali na kuanzisha ushirikiano mpya unaolenga kukifanya kilimo kuwa kuwa chenye faida na cha kibiashara. “Ushirikiano huu na AGRA umekuwa wenye faida kwa ongezeko la ukuaji wa uzalishaji mazao ya kilimo nchini. 
Tuna imani kwamba kupitia makubaliano mapya, tutakuwa na rasilimali na uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi: si kwa utoaji fedha tu bali utoaji wa mbinu mahususi za kilimo,” alisema Dk Kalibata .
Aliongeza, “Tanzania ina uwezo mkubwa wa kukuza kilimo chake kiasi cha kuwanufaisha mamilioni ya wakulima wadogo na kuboresha maisha yao na kuwapo usalama wa chakula.” Kupitia makubaliano mapya, AGRA na serikali wataainisha maeneo ya vipaumbele kwa rasilimali na ukuaji wa kilimo. AGRA na washirika wake watatoa misaada ya fedha na mbinu bora za kilimo.
Pia, mkataba mwingine ulisainiwa ukilenga utekelezaji wa mradi wa mageuzi madogo ya kilimo biashara barani Afrika (Mira). 
Miezi michache iliyopita, teknolojia mpya ya kuhifadhi mazao ilizinduliwa kwa ushirikiano wa AGRA na taasisi ya Rockefeller kwa wakulima wa Ruvuma, Mbeya na Njombe ambayo imechangia tofauti kubwa ya kuzuia upotevu wa mbegu zenye thamani ya mabilioni ya Shilingi kwa maelfu ya wakulima wadogo.

No comments:

Post a Comment