Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (kushoto) na Mchungaji Ngwandu Mwangasa wakitoka katika Kituo Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Wakili wa Askofu Gwajima, John Mallya
Dar es Salaam. Sasa ni dhahiri kwamba polisi
wamemshika pabaya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
baada ya kumhoji na kisha kumtaka arejee katika Kituo Kikuu cha Polisi
Dar es Salaam Aprili 16, mwaka huu akiwa na vitu 10 vinavyohusu usajili,
umiliki, uongozi na mali za kanisa analoliongoza.
Hatua hiyo imekuja kinyume na matarajio yake na ya
wengi kuwa kiongozi huyo angekuwa anahojiwa tu kuhusu matamshi yake ya
kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo.
Kutokana na matamshi hayo yaliyosambaa kwa kasi
kwenye mitandao ya kijamii kwa njia ya video na sauti, Gwajima alitakiwa
kuripoti polisi kuhojiwa Machi 27, mwaka huu lakini kabla ya mahojiano
yao kukamilika aliishiwa nguvu na kupelekwa hospitalini alikolazwa kwa
siku nne, huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa na kuhojiwa taarifa
binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa polisi.
Hata baada ya kutoka hospitalini, Gwajima
aliendelea kutembea akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alichotumia
hadi Aprili 6 alipohubiri katika Ibada ya Pasaka.
Siku iliyofuata askofu huyo alitupa kiti hicho
akidai kuwa amepona baada ya maombi ya wachungaji wageni waliofika
kanisani hapo kutoka Japan.
Baada ya mahojiano ya jana, wakili wake, John
Mallya alilalamikia hatua ya polisi akisema mahojiano kuchukua mkondo wa
mambo binafsi badala ya kile alichoitiwa na kusema watakwenda
kulalamikia hatua hiyo mahakamani.
Mambo 10
Wakili huyo alitaja mambo yanayotakiwa
kuwasilishwa polisi kuwa ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili,
majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa
(matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa, muundo wa uongozi
wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za
nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa
Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za
video kanisani hapo.
Mallya alisema watalalamika suala hilo
litakapofika mahakamani kutokana na mteja wake kuhojiwa masuala tofauti
na kile kinachodaiwa kutoa lugha ya matusi.
Alisema mteja wake amehojiwa muda mrefu kwa sababu
alikuwa akihojiwa masuala binafsi yakiwamo ya familia yake, watoto
wake, ndugu zake hadi waliokufa.
“Mahojiano yamekuwa ya muda mrefu, cha kushangaza
kaulizwa maswali binafsi badala ya kile anachodaiwa kukifanya,
mahakamani tutahoji hilo,” alisema Mallya.
Alisema licha ya kuambiwa walete vitu hivyo ambavyo kimsingi vipo, hawajaambiwa watafanywa nini kama wasipoviwasilisha.
Saa 1.15 asubuhi akiwa ameongozana na watu wawili akiwamo
msaidizi wake ambaye alikuwa amemshikilia kutokana na kutembea kwa
kupepesuka na wakili wake Malya, Gwajima alionekana akikunja uso kila
alipopandisha ngazi moja kwenda nyingine kuelekea ndani ya Kituo Kikuu
cha Polisi.
Baada ya kukaa ndani hadi saa 6.45 mchana, Gwajima
alitoka akiwa ameshikiliwa kama alivyoingia na kuzungumza na waandishi
wa habari na kusema mahojiano yalikwenda vizuri kuliko walivyotarajia,
huku akimtaka wakili wake kufafanua zaidi, ndipo wakili huyo alipotaja
mambo hayo.
Katika eneo la polisi, wafuasi wa Gwajima walikuwa
katika makundi na ilipofika saa 1.40 asubuhi, Kamishna Msaidizi wa
Polisi, Simon Sirro aliwaita wapatao 20 miongoni mwao na kuwaliza
wanachotaka, nao wakamjibu bila hofu kuwa wamemfuata baba yao.
Sirro aliwataka waumini hao waondoke akiwaeleza
kuwa baba yao yupo katika mikono salama na wao waende wakafanye kazi za
kutafuta mkate wa siku.
Hata hivyo, waumini hao walimjibu kuwa hawaondoki
hadi baba yao atakapotoka na wao ndipo watakapoondoka.” Majibu
yaliyomuacha hoi na kumfanya kucheza na kisha kuondoka kurejea ofisini
kwake huku akisema... “Makubwa.”
Waumini hao walikuwa wakiongezeka kadri muda
ulivyokwenda na hadi saa tano walikuwa wengi katika makundi wakiwamo
walinzi shirikishi ambao walipata mafunzo kwa ufadhili wa Gwajima, ambao
walikuwa wamejipanga langoni mwa kituo hicho wakiwa watulivu.
Waumini wazungumza
Wakizungumza kituoni hapo, waumini hao walisema
wamepita mapito mengi na kiongozi huyo hivyo ni vigumu kumuacha peke
yake katika eneo ambalo alipata matatizo mara ya kwanza.
Mmoja wao, Eugen Mkwasa alisema hajakwenda katika
biashara zake kwa sababu ya kulinda usalama wa baba yao, kwa kuwa hana
imani na eneo alilokuwapo kwani ndilo lililokuwa chanzo cha mateso yake
ya sasa.
“Askofu wetu mpendwa anaumwa, hali hiyo ilimuanza
akiwa hapa kituoni, nitakuwa na raha gani kubaki nyumbani au kwenda
kibaruani bila kufahamu kama baba ametoka salama?” alisema Mkwasa.
Muumini mwingine, Elizabeth Peter alisema hajali
jua na hata ikinyesha mvua kwa sababu analipa kile anachotendewa na
Askofu Gwajima... “Askofu tumepita naye katika mapito mengi, siwezi
kukaa mbali na suala lake kwa sababu ana mchango mkubwa maishani mwangu,
siwezi kumtupa wakati huu mgumu wa kusumbuliwa na Jeshi la Polisi.”
No comments:
Post a Comment