Sunday, 12 April 2015

Askofu Gwajima ajipalia makaa

Josephat Gwajima
Joseph gwajima

HATUA ya mawakili wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kutengeneza ubishi wa kisheria katika agizo la Polisi la kuwasilisha nyaraka za mali za Askofu huyo, imeelezwa kuwa ni ukaidi ambao hautamsaidia kisheria. Badala yake, kwa hatua hiyo ya mawakili hao, Jeshi la Polisi limewekewa mazingira mazuri ya kuchukua hatua ya pili ya matumizi ya nguvu katika kutekeleza agizo lao, baada ya hatua ya hiyari kushindikana. Wakizungumza na gazeti hili jana, wanasheria mbalimbali walishangazwa na ubishi wa juzi, uliotokana na barua ya mawakili wa Askofu Gwajima kwenda kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Katika barua hiyo, mawakili hao walitaka Polisi itoe agizo la maandishi la kuwasilisha nyaraka hizo, litakaloeleza vifungu vya sheria vinavyomtaka mteja wao kuwasilisha nyaraka hizo. Ukaidi wa Gwajima Barua hiyo iliyosainiwa na Wakili Peter Kibatala, iliwasilishwa juzi mchana katika jeshi hilo ikiwa ni siku moja baada ya Askofu Gwajima kutakiwa kuwasilisha nyaraka 10 zinazohusu umiliki wa mali zake, Aprili 16 mwaka huu watakapoendelea na mahojiano. Mawakili hao kwa niaba ya mteja wao wameliomba Jeshi la Polisi kumwandikia barua rasmi Gwajima, wakiainisha nyaraka wanazozihitaji, pamoja na vifungu vya sheria vinavyotumiwa na jeshi hilo kutaka nyaraka hizo. Mawakili hao wanasema watashukuru kupata hati hiyo ambayo wamedai hawaijui jina, lakini wanaamini Jeshi la Polisi litafahamu jina la kisheria la nyaraka husika inayotumika kumtaka Gwajima, awasilishe nyaraka wanazozihitaji. Aidha wanasema askofu Gwajima atakapopata nyaraka anayoihitaji, atatimiza mwito na kuchukua hatua stahiki za kisheria. Nyaraka 10 Nyaraka hizo ni Hati ya Usajili wa Kanisa, Namba ya Usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya Kanisa na muundo wa uongozi wa Kanisa. Nyingine ni Waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za Kanisa na nyaraka zinazoonesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari. Pia waliagizwa kufuatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo. Ushauri Wakifafanua kuhusu ubishi huo wa kutaka sheria inayotumiwa na Polisi kuagiza nyaraka hizo, wanasheria waliozungumza na gazeti hili walisema hakuna sheria yoyote inayomzuia Polisi kudai umiliki halali wa mali au nyaraka endapo watazihitaji. Mwanasheria Dk Damas Ndumbaro, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai na ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, askari Polisi amepewa fursa ya kufanya ukaguzi wa mali na nyaraka zozote bila ya kuzuiwa na mtu. ‘’Polisi anaweza kufanya ukaguzi nyumbani kwako bila kuwa na hati ya ukaguzi na anaweza kuwa nayo. Lengo lao ni kukamilisha masuala yao ya kipolisi tu,’’ alisema mwanasheria huyo Pia alisema Polisi wanaweza kuagiza mtu yeyote ambaye wanamtilia shaka, apeleke mali au taarifa zozote ambazo wanaamini kwamba zitawasaidia katika kukamilisha upelelezi. Kwa upande wake, Mwanasheria Emmanuel Makene, alisema kama Gwajima anamiliki kihalali mali ambazo Polisi wametaka kujua uhalali wake, hawezi kuwa na wasiwasi na anachotakiwa ni kutii. Mkono wa dola Makene alisema endapo Gwajima au mtu yeyote akitakiwa kupeleka nyaraka za mali akakaidi amri hiyo, Polisi wanaweza kutumia nguvu dhidi yake. Aliongeza kuwa mtu yeyote hawezi kujua ni kwanini Polisi wanachunguza na kwa kuwa wana haki na wala hakuna sheria inayowazuia, lazima wafuate sheria. ‘’Kwa mfano, mara nyingi tunaona madereva wanasimamishwa na askari wa Usalama Barabarani na kumtaka atoe leseni yake ama bima, mbona watu wanakubali kutoa vitu hivyo? ‘’Trafiki huyo anaweza kufanya hivyo kwa kukutilia shaka kwani inawezekana kwenye leseni yako kuna jina la mwanamke, halafu unayeendesha gari au pikipiki ni mwanamume, ni lazima Polisi ahoji uhalali wa mali unayoiendesha barabarani,’’ alifafanua Makene. Aliendelea kufafanua kuwa, mtu mwema hawezi kukataa kuhojiwa au kuchunguzwa na kama kitu kinachotakiwa ni chake hawezi kuogopa. Makosa ‘mazito’ Akizungumzia suala la Askofu Gwajima, Ndumbaro alisema kuwa huenda askari Polisi wanamtilia shaka kupitia mambo mawili, ikiwamo utakatishaji wa fedha. ‘’Hatua ya Polisi kudai nyaraka za umiliki wa mali za Askofu Gwajima, huenda wanatilia shaka masuala ya utakatishaji wa fedha au ugaidi,’’ alisema Ndumbaro. Alifafanua kuwa huenda Polisi wanataka kujua ni njia gani amezitumia Askofu Gwajima katika kujenga kanisa lake hadi lilipofikia. ‘’Watu wengi wanataka kujua uhalali wa makanisa yanayojengwa hivi sasa. Tatizo lilikuwepo katika makanisa mengi nchini kujihusisha na masuala ya utakatishaji wa fedha na hivyo ni halali kuhoji ili iwekwe wazi ni vipi yamejengwa,’’ alisema. Sakata la Askofu Gwajima lilianzia katika matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Kutokana na matamshi hayo yaliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii kwa njia ya video na sauti, Gwajima alitakiwa kuripoti Polisi kuhojiwa Machi 27, mwaka huu. Hata hivyo kabla ya mahojiano yao kukamilika, Askofu Gwajima aliishiwa nguvu na kupelekwa hospitalini alikolazwa kwa siku nne, huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa baada ya kuhojiwa taarifa binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa Polisi. Hata baada ya kutoka hospitalini, Askofu Gwajima aliendelea kutembea akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alichotumia hadi Aprili 6 mwaka huu alipokuwa akihubiri katika Ibada ya Pasaka. Siku iliyofuata Askofu huyo alitupa kiti hicho akidai kuwa amepona baada ya maombi ya wachungaji wageni waliofika kanisani hapo kutoka Japan

No comments:

Post a Comment