Rafiki,
Najua tangu tarehe 09/11/2016 umeshasikia mengi sana kuhusu Donald Trump, umeshaandikiwa na kusoma mengi kuhusu ushindi wake kwenye uchaguzi wa uraisi na kumwezesha kuwa raisi wa taifa kubwa duniani, Marekani.
Naomba nikuahidi kwamba hapa nitakwenda kukushirikisha mambo ambayo ni mageni kabisa, mambo haya hujayasikia popote, na kama umeyasikia basi hapa utayasikia kwa njia ya tofauti. Nitakwenda kukushirikisha hatua za wewe kuchukua ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Jinsi nilivyomjua Donald Trump.
Katika harakati zangu za kusoma vitabu, mwaka 2012 nilikutana na kitabu NEVER GIVE UP, ambacho kimeandikwa na Donald Trump.
Katika kitabu kile, alieleza jinsi alivyofilisika na kibiashara na kuwa na deni kubwa, lakini akaweza kupambana na kurudi kwenye game na kuwa bilionea. Nilijifunza mengi kibiashara na kijasiriamali kupitia namna anavyoendesha biashara zake.
Baadaye nikasoma kitabu chake kinaitwa ART OF THE DEAL, hapa nilijifunza mengi sana ya namna ya kuweza kupata chochote unachotaka. Na namna biashara nyingi zilivyo kama vita.
Nimesoma pia vitabu vyake viwili alivyoshirikiana na Robert Kiyosaki, MIDAS TOUCH ambacho kinaelezea safari ya ujasiriamali na WHY WE WANT YOU TO BE RICH ambapo wameandika mbinu za kufikia uhuru wa kifedha.
Nimesoma vitabu vyake vingine viwili; THINK LIKE A BILLIONARE na THINK LIKE A CHAMPION.
Kupitia kila kitabu kuna mengi nimejifunza kuhusu safari ya mafanikio, hasa kwenye biashara na ujasiriamali. Nikazielewa falsafa zake na nikavutiwa naye.
Nikamweka Donald Trump kwenye orodha yangu ya watu 100 ambao nawaita MENTORS wangu. Hawa ni watu ambao najifunza mengi kupitia maisha yao.
Mwaka jana wakati anatangaza kugombea uraisi wa marekani, nilifurahishwa sana na nikapanga kumtoa kwenye list ya MENTORS, kuingia kwenye list yangu ndogo ya ROLE MODELS wangu (kwa sasa wapo watatu, Seneca, Elon Musk na Wiston Churchill).
Kwa sababu alikuwa na sifa mbili ambazo ndiyo napigania mimi. Kwanza ni bilionea (malengo yangu ni kuwa bilionea kabla sijatimiza miaka 40) na anakwenda kugombea uraisi (Malengo yangu ni kuwa raisi wa Tanzania mwaka 2040).
Niliona nina mengi sana ya kujifunza kwake, kwa sababu kwa namna nilivyokuwa nimemfahamu kupitia maandiko yake, sikuwa na shaka kwamba anaweza kushindwa.
Lakini baada ya kampeni kuanza, kuna vitu sikupenda kuiga kutoka kwake, hivyo nikamtoa kwenye orodha ya ROLE MODELS na akabaki kwenye orodha ya MENTORS.
Nachukua nafasi hii kumpongeza sana na kuishangaza dunia kwa sababu ni kitu ambacho hakikutegemewa kabisa. Japo yeye na wachache wengine walikuwa wakijua ushindi ni lazima.
Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa Donald Trump, na kuna mengi pia ya kuepuka kutoka kwake.
Yafuatayo ni mambo kumi muhimu ya kujifunza kupitia Raisi Mteule wa Marekani, Donald Trump.
1. Kuwa na maono makubwa yanamvutia kila mtu.
Tangu Trump anatangaza kugombea uraisi wa Marekani, amekuwa na maono makubwa kwa nchi yake, ambayo ni rahisi kwa mtu yeyote kuyaelewa na kutamani kuwa sehemu ya maono hayo. Maono yake yalibebwa na kauli MAKE AMERICA GREAT AGAIN.
Yaani IFANYE AMERIKA KUWA KUBWA TENA. Kila alipokuwa huu ndiyo ulikuwa ujumbe, na alionesha ni namna gani Amerika imepoteza ukuu wake. Kila mtu anapenda ukuu na kila mtu anapenda kuwa sehemu ya ukuu. Wengi walimwamini kwa maono haya na kupenda kuwa sehemu ya maono haya.
2. Jua ni nini hasa unachotaka.
Ukiangalia maisha ya Donald Trump, biashara zake na hata mchakato mzima wa kugombea uraisi wa marekani, alijua kwa hakika ni kitu gani hasa anachotaka. Alijua anataka kuwa raisi wa Marekani na anachotaka ni ushindi pekee, siyo kujaribu, bali kushinda. Kwa kulijua hili na kuweka juhudi, hatimaye ameweza kushinda.
3. Weka juhudi kubwa kwenye kile unachotaka.
Ukiangalia mambo mengi ambayo amekuwa anafanya Trump, na hata huu uchaguzi alioshinda, amekuwa siyo mtu wa kujaribu. Amekuwa anafanya kwa kuamini atashinda na hivyo kuweka juhudi zake zote. Amekuwa hasubiri mambo yatokee, badala yake amekuwa anayafanya yatokee. Amekuwa tayari kujitoa hata kwa hatua ya ziada ili kupata kile anachotaka.
4. Jiamini kwamba unaweza na hakuna cha kukushinda.
Kama kuna kitu kimoja ambacho Trump anacho, basi ni kujiamini. Amejiamini kupita kiasi na hili limekuwa linawakera wengi. Ni kujiamini kwake huku ambapo kumewafanya wengi pia wamwamini na hatimaye kushinda uchaguzi. Moja ya kauli alizonukuliwa akisema ni hii; sijawahi kushindwa, maisha yangu yametawaliwa na ushindi. Kujiamini huku kunawafanya wengi kumwona kama ni mtu asiye wa kawaida.
5. Vyombo vya habari vina ajenda binafsi.
Ukiangalia mchakato mzima wa uchaguzi wa Marekani, vyombo vya habari vimekuwa vinampinga sana Trump. Vimekuwa vinatoa upendeleo wa wazi kwa mgombea mwingine na kukuza mambo hasi ya Trump. Vyombo karibu vyote vya habari vilitumia muda mwingi kumshusha Trump lakini vimeshindwa.
6. Maoni na ukweli ni vitu viwili tofauti.
Wakati wa uchaguzi, zilipigwa kura nyingi za maoni, na zote zilionesha Trump atashindwa. Kutokana na kura hizi karibu kila mtu aliona hakuna namna Trump ataweza kushinda. Lakini mwishowe ameshinda. Hii inatuonesha ni namna gani maoni hayaendani na ukweli na uhalisia.
7. Tumia muda mwingi wa kutangaza mazuri yako na siyo mabaya ya mwenzako.
Mgombea aliyepewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa Marekani, Hillary Clinton, alitumia muda mwingi kuonesha mabaya na madhaifu ya Trump. Alikuwa akiwasihi sana Wamarekani wasimchague Trump kwa sababu atakua kiama kwa nchi yao. Walilipia matangazo mengi yakionesha madhaifu ya Trump. Japo pia Trump alifanya hivi kwa mwenzake, lakini alitumia muda mwingi zaidi kuelezea mazuri yake na kwa nini watu wamchague yeye.
8. Unapokosea, kubali, omba radhi na songa mbele.
Katika kipindi chote cha kampeni, yapo makosa mengi aliyofanya Trump, pia yapo makosa yake mengi ya nyuma yaliyoibuliwa kwenye kampeni. Moja ya makosa hayo ni mkanda wa video ukionesha akiongea kudhalilisha wanawake. Baada ya mkanda ule kutoka kila mtu alikata tamaa na Trump, kila mtu alijua habari yake imeisha. Lakini siyo yeye, alipoulizwa kuhusu mkanda huo alikiri i yeye ameongea na alikosea, anaomba asamehewe maana alishajifunza. Kwa kukubali huku na kuomba msamaha kulifanya habari ile isiwe kubwa na kumharibia zaidi.
9. Huwezi kumjua vizuri mtu kama hujamwona kwenye nyakati mbalimbali.
Nimemjua Trump tangu mwaka 2012 nilipoanza kusoma vitabu vyake. Niliona nimeshamjua kupitia maandiko yake na namna alivyokuwa anaendesha maisha yake. Lakini nimekuja kujua mengi zaidi wakati wa mchakato wa kugombea uraisi. Yapo mengi ambayo sikuyajua kuhusu yeye hapo awali. Yapo mengi ambao sitapenda kuyaiga kutoka kwake, japo yamemsaidia kupata ushindi kwenye uchaguzi.
10. Kamwe usikate tamaa, kamwe kamwe usikate tamaa.
Hii hata Trump mwenyewe ameiandika kwenye kitabu chake cha NEVER GIVE UP. Trump amepitia magumu mengi kwenye maisha yake, lakini hajawahi kukata tamaa. Hata wakati huu wa uchaguzi, kila mtu alimkataa, viongozi wa chama chake walimkataa, hata maraisi waliostaafu wote walimkataa na kusema hafai na hawezi kuwa raisi.
Wataalamu wa mambo ya siasa walimkataa na kusema hawezi kuwa raisi, hawezi kushinda. Kila kura ya maoni ilionesha akishindwa. Lakini Trump hakusikiliza hayo, badala yake aliendelea kuweka juhudi kubwa, na mwisho wa siku ameibuka mshindi.
Ukishafanikiwa kila mtu anakuchukulia hasi.
Moja ya vitu vilivyofanya watu wengi kumchukulia hasi Donald Trump ni mafanikio yake makubwa. Trump ni Bilionea, ambaye utajiri wake unakadiriwa kufikia dola bilioni 4 za kimarekani. Kuna misingi ambayo amekuwa anaiishi ndiyo maana akaweza kufikia mafanikio haya. Sasa baada ya kufanikiwa, wengi wanachambua misingi yake kwa upande hasi. Wengi wanachukua madhaifu yake na kuyakuza zaidi.
No comments:
Post a Comment