Friday, 3 March 2017

Serengeti Boys kunolewa na Nyota wa Liverpool

JOHN BARNES.
Mchezaji mkongwe wa Liverpool ya England, John Barnes, amewasili nchini jana kwa ajili ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za michezo ikiwamo kuwafunda wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana ya umri chini miaka 17 (Serengeti Boys).
Barnes amekuja nchini kwa mwaliko wa Benki ya Standard Chartered ambayo kesho itasheherekea miaka 100 tangu ilipoanzishwa mwaka 1917.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Sanjay Rughani, alisema anaamini ujio wa nyota huyo utasaidia kuhamasisha wachezaji chipukizi kufikia malengo yao kwa kuwa wachezaji wa kimataifa.
Rughani amesema amefurahi kuona timu kutoka sehemu mbalimbali zilichuana kuwania Kombe la Standard Chartered ambalo mabingwa wake wataenda kutembelea makao makuu ya Liverpool na kushuhudia wakicheza mechi mojawapo ya Ligi Kuu England.
Alisema mbali na kumualika mkongwe huyo, benki yao inajipanga kusaidia maandalizi ya Serengeti Boys ambayo baadaye mwaka huu itashiriki fainali za Afrika za Vijana zitakazofanyika Gabon.



Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema kuwa wanaamini mazungumzo atakayofanya mchezaji huyo yatawasaidia kiufundi wachezaji wa Serengeti Boys ambao wanatarajia kuchuana na wenzao wenye uzoefu wa kucheza michuano mbalimbali ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment