Na Eleuteri Mangi
Maafisa Mawasiliano Serikalini
wametakiwa kuendelea kuitendea haki taaluma yao kwa kuhabarisha na
kuisemea Serikali juu ya utoaji huduma za jamii na utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel
kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi wakati wa
kufunga Kikao Kazi cha mwaka cha Maafisa Mawasiliano Serikalini mjini
Dodoma.
“Mtaheshimika kwa kuiambia jamii
na kuwapa taarifa kwa wakati. Nguvu ya habari ni kubwa, muitumie vizuri
kwa kuongeza thamani ya kazi zenu na wafikisheni viongozi wenu kwenye
mafanikio ya malengo yaliyowekwa ambapo uwepo wenu utasaidia kwa mchango
wako wa kuwa mbunifu katika kutekeleza majukumu yako” alisema Prof. Ole
Gabriel.
Prof. Ole Gabriel aliwahimiza
Maafisa hao kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa habari kwa
manufaa ya Watanzania kwa kuzingatia Sheria za nchi ikiwemo Sheria ya
Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi amesema kuwa ili Vitengo vya Mawasiliano Serikalini viweze
kuuhabarisha Umma kwa wakati ni lazima kuwe na mawasiliano ya kimkakati
ambayo yatasaidia kuisemea Serikali kwa wananchi wake katika mambo
mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali yao.
Dkt. Abbasi aliongeza kuwa ili
kufikisha taarifa kwa umma kwa wakati zipo njia kuu ambazo zinaweza
kusaidia kufikia malengo ya mawasiliano ya kimkakati katika kuhabarisha
umma ikiwemo kuweka malengo makubwa.
“Rais Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipoweka lengo la ununuzi wa Ndege
ilionekana inawezekana vipi? Matokeo yake ndege mpya aina ya Bombardier
zipo na zinafanya kazi nchini,haya ni matokeo ya malengo makubwa
aliyojiwekea, nasi tufanye hivyo katika tasnia ya habari” alisema Dkt.
Abbasi.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi
kufunga kikao kazi hicho, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nuru Millao
aliwataka Maafisa Mawasiliano kuandika habari na makala za miradi
mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali pamoja na kufuatilia
na kujibu ya hoja na kero za wananchi kwa wakati kwa kushirikiana na
Idara ya Habari (MAELEZO) ambayo ndiyo kiunganishi cha Vitengo vya
Mawasiliano Serikalini nchini.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha
Maafisa Mawasiliano ya Serikalini (TAGCO) Paschal Shelutete amemuahidi
Mgeni Rasmi kwa niaba ya Washiriki wa Mkutano huo kuwa watayafanyia kazi
maagizo yaliyotolewa pamoja na maazimio yaliyofikiwa katika mkutano
huo na kufanya kazi kwa weledi na kwa wakati ili kuhakikisha kazi za
Serikali zinafahamika kwa Umma wa Watanzania.
Mkutano huo ulihudhuriwa na jumla
ya washiriki wapatao 231 kutoka Wizara mbalimbali, Idara za Serikali,
Taasisi, Wakala, Miji, Majiji, Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment