Mkazi wa Dar es Salaam Bw.
Michael Francis baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au
kulipa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la udanganyifu katika
huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Mshitakiwa wa Pili na wa Tatu wakiwa chini ya ulinzi baada ya kutiwa hatiani na kuhumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
Mshitakiwa Bw. Francis muda mfupi baada ya kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya udanganyifu.
Mshitakiwa Bw. Godfrey Nyika
ambaye ndiye kitambulisho chake cha matibabu kilitumiwa isivyo halali na
BW. Francis baada ya hukumu.
Na Grace Michael
Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya
ya Kinondoni imewahukumu wakazi wawili wa Mkoa wa Dar es Salaam kifungo
cha miaka miwili jela au faini ya shilingi Milioni moja kwa makosa ya
kujipatia huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa njia za
udanganyifu.
Hukumu hiyo imetolewa leo
mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mwandamizi Bweguge Obadia ambaye alisema
kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashitaka
umeithibitishia mahakama pasipo shaka ya aina yoyote kuwa washitakiwa
hao walitenda makosa hayo.
Waliohukumiwa kifungo hicho ni
pamoja na Bw. Michael Francis na Bw. Godfrey Nyika ambao ni washitakiwa
wa pili na wa tatu huku mshitakiwa wa kwanza Bw. Rashid Kidumule
akiaachiwa huru baada ya kuthibitika kutotenda kosa hilo.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi
Mwandamizi Bw. Obadia alisema kuwa hakuna shaka yoyote juu ya
washitakiwa hao kutenda makosa ya kujiwakilisha katika duka la dawa la
Nakiete kwa lengo la kujipatia huduma ya dawa kwa kutumia kitambulisho
cha matibabu cha mshitakiwa wa tatu ambaye ni Bw. Nyika.
“Ushahidi wa mashahidi wa
mashitaka unathibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa mshitakiwa wa pili
Bw. Francis alijiwakilisha dukani kwa lengo la kupata dawa kwa kutumia
kadi isiyo yakwake na hakuna shaka kuwa mshitakiwa wa tatu ambaye ndiye
mwenye kadi alimpatia kadi hiyo mshitakiwa wa pili hivyo kwa ushahidi
huu Mahakama inawatia hatiani,”anasema Hakimu Mkazi Bw. Obadia.
Alisema kuwa Mahakama hiyo
imezingatia makosa waliyoshitakiwa nayo washitakiwa hao pamoja na
uhusika wao katika kutenda makosa hayo. Kutokana na hali hiyo, Mahakama
ilimhukumu Bw. Francis kifungo cha miaka miwili jela au faini ya
shilingi milioni moja huku mshitakiwa Bw. Nyika akihukumiwa kifungo cha
mwaka mmoja au faini ya shilingi laki tano.
Washitakiwa hao walitenda makosa
hayo ya kujiwakilisha kwa lengo la kujipatia huduma mwaka 2014 ambapo
kesi hiyo imehitishwa kwa wao kukutwa na hatia na kuhukumiwa adhabu
hiyo.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya
umekuwa ukitahadharisha wanachama wake juu ya matumizi ya vitambulisho
vyao vya matibabu kwa kuonya kufanya udanganyifu wa aina yoyote kwenye
huduma zake.
Akizungumza na Mwandishi wa
habari hizi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw.
Bernard Konga amesema Mfuko utaendelea kuchukua hatua stahili kwa
wanachama wasio waaminifu ambao watajihusisha na udanganyifu wa aina
yoyote.
“Nitoe tu tahadhari kwa wanachama
na watoa huduma wote kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuulinda Mfuko kwa
kuhakikisha huduma anayoitoa au kuipata iko katika njia sahihi, Mfuko
hautakuwa tayari kufumba macho kwa wanaojihusisha na udanganyifu au
kuhujumu Mfuko kwa namna yoyote,” alisema Bw. Konga.
No comments:
Post a Comment