Baadhi ya maduka
Kibamba wilaya ya Ubungo yakionekana kubomolewa katika zoezi la bomoa
bomoa ili kupisha upanuzi wa barabara ya kwenda Katika ofisi za
halmashauri ya wilaya ya Ubungo na hifadhi ya barabara. (Picha na
Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi
Serikali imeanza zoezi
la bomoa bomoa nyumba za biashara na makazi ya watu 110, katika mtaa wa
Kibamba halmashauri ya wilaya ya Ubungo waliojenga katika hifadhi ya
barabara.
Zoezi hilo lililoanza
jana ambapo linalenga kuvunja jumla ya nyumba hizo ili pia kupisha
upanuzi wa barabara ya kwenda kwenye ofisi za halmashauri ya wilaya mpya
ya Ubungo.
Meneja wa TANROAD Dar
es salaam, Julius Ndyamukama akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu,
alisema kuwa mbali ya upanuzi wa barabara hiyo ya kwenda halmashauri ,
bomoa bomoa hiyo itawakumba na wale waliowekewa alama ya X na kupuuza na
kuamua kuendeleza majengo yao.
Aliwashauri wananchi kutii sheria za nchi ili kuepuka adha ya kubomolewa.
Ndyamukama aliwataka
wananchi wajenge katika maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya ujenzi wa
makazi badala ya kujenga katika hifadhi ya barabara kama ilivyo sasa.
Baadhi ya wananchi
waliokumbwa na bomoa bomoa akiwemo Adamu Mbonde, Shanifa Ngoma, Grace
Lusasa , wameitupia lawama serikali kwa kushindwa kutoa notisi ili
waweze kujiandaa na kuhamisha mali zao ili zisiharibiwe.
Walisema kwanza hawajapewa notisi wala kupewa muda wa kujipanga kuhama.
Shanifa alielezea kuwa
hakuna aliyekataa kuhama tatizo ni kubomolewa pasipo serikali kujali
athari wanayopata wananchi ikiwemo kushindwa kutoa mabati, matofali na
vifaa kutokana na tanesco kutozima umeme ili watoe mali zao.
“Tumepata hasara kubwa
ya upotevu wa mali na bidhaa kwani zingine ziliharibika kutokana na
kuhamisha kwa haraka na zingine ziliharibiwa na katika bomoabomoa hiyo ”
alisema Shanifa.
Alifafanua kuwa wengine
hawakuwekewa alama ya X lakini wamebomolewa bila taarifa wala kupewa
muda kisa kupisha barabara ya kwenda ofisi za halmashauri ambayo
inatumiwa pia na mkuu wa wilaya ya Ubungo.
Nae diwani wa kata ya
Kibamba Ernest Mgawe, alikiri kuwepo kwa bomoa bomoa katika kata yake
lakini ameitupia lawama TANROAD kwa kushindwa kuwapa taarifa kwa
maandishi na kutopewa muda.
Kwa mujibu wa diwani
huyo anasema wananchi wake wamekosa muda wa kutosha wa kujiandaa hivyo
sheria na taratibu zingefutwa na kujali maslahi ya wananchi.
Enerst alielezea kwamba wangearifiwa ili wahamishe mali zao bila kupata hasara.
No comments:
Post a Comment