Uzinduzi wa
Ligi ya Taifa ya Wanawake unatarajiwa kufanyika Novemba 1, 2016 kwenye
Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma katika mchezo ambao Baobao itacheza na
Victoria Queens ya Kagera.
Ligi hiyo ya kwanza kufanyika
nchini Tanzania, lakini pia kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati
imetokea kuvutia wadau kadhaa wakiwamo Azam Tv ambao wamedhamini kwa
kuonyesha mubashari (live), michezo hiyo 30 itakayofanyika viwanja
mbalimbali.
TFF imepeleka uzinduzi huo Dodoma
ikiwa na lengo la kuhamasisha soka mikoani tofauti na Dar es Salaam
ambako ilizoeleka zaidi miaka ya nyuma kabla ya kuwa na mpango wa
mashindano ya aina hiyo yanayoshirikisha timu 12 kutoka kona mbalimbali
za nchi.
Kadhalika, kwa siku ya Novemba
mosi ya uzinduzi huo vingozi wengi wa Serikali wakiwamo wabunge
wanatajiwa kuwa Dodoma ambako watapata fursa pekee ya kushuhudia
burudani ya mpira wa miguu wa ushindani itakayosukuma hamasa ya kutoa
michango yao mbalimbali kwa ajili ya soka la wanawake.
Mbali ya mchezo huo wa kundi B
kati ya Baobao na Victoria, michezo mingine itakuwa ni kati ya Sisterz
na Panama utakaofanyika Uwanja wa Tanganyika huko Kigoma wakati Marsh
Academy ya Mwanza itacheza na Majengo Women ya Singida kwenye Uwanja wa
CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kundi A kutakuwa na michezo mitatu
ambako Viva Queens ya Mtwara itacheza na Mburahati Queens ya Dar es
Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Fair Play ya Tanga
itapambana na Evergreen ya Dar Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja
wa Mkwakwani mjini Tanga huku JKT Queens ikiwa ni wenyeji wa Mlandizi
Queens ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment