Kongamano
la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu za soka limefanyika Jumamosi
Oktoba 22, 2016 kwenye ukumbi wa Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam.
Kongamano
hilo lililoandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzani
(TASWA) lilishirikisha wadau zaidi ya 60 nchini.
Kituo cha televisheni cha Azam kilionesha live (mubashara) kongamano hilo huku wajumbe wakikubaliana masuala kumi ya msingi.
Kwanza
wajumbe walikubali kuwa kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko sasa kwa
sababu muundo unaotumika kuendesha klabu za soka una matatizo mengi.
Pili
iliamuliwa klabu zijiandae vya kutosha kukaribisha mabadiliko hayo
ikiwa ni pamoja na kuboresha utawala bora (governance) kwenye uendeshaji
wa klabu.
Tatu
mifumo yetu kama nchi inawezesha klabu kuwa na aina nyingi za mifumo ya
kiuendeshaji hivyo wanachama waelimishwe kwa kina kuhusu mifumo hiyo
ili wachague ulio bora zaidi kwa manufaa ya klabu zao.
Nne ili mabadiliko haya yafanyike kwa haki, inatakiwa wamiliki wa timu hizi (wanachama) waelimishwe vya
kutosha juu ya thamani yao ili wajitambue. Kwamba thamani ya klabu
kubwa nchini haiwezi kulinganishwa na kiasi cha fedha kinachotolewa na
wawekezaji hivyo wanachama wasiingie kwenye mabadiliko wakiwa wanyonge
kwa sababu wao ndio wana mtaji mkubwa kuliko hela zinazoletwa kwa ajili
ya uwekezaji.
Tano
mabadiliko haya hayawezi kufanywa na wanachama na wawekezaji pekee bila
kuishirikisha serikali. Hivyo klabu zinapojipanga kwa mabadiliko haya
zihakikishe zinashirikisha serikali na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).
Sita mabadiliko haya yasifanywe kishabiki bali yafanywe kitaalamu ili kutengeneza msingi Imara utakaoepusha migogoro hapo baadaye.
Saba
kuelekea mabadiliko haya, hasa katika kipindi hiki ambacho uelewa wa
wanachama ni mdogo, serikali inatakiwa kulinda maslahi ya walio wengi
kwa kuingilia kati pale inapoona kuna mwelekeo wa kuwa na mabadiliko
yanayominya maslahi ya walio wengi.
Nane
mpira ni biashara ya kipekee ambayo mafanikio yake yanategemea jinsi
washindani wanavyoshirikiana. Hivyo kuelekea mabadiliko haya wanatakiwa
watumike wataalamu wa biashara ya mpira ili klabu zinapobadilika ziweke
misingi itakayokubaliana na biashara ya soka.
Tisa klabu
zinao wajibu wa kulinda hadhi zake (brand) kwa sababu eneo hilo ndio
msingi wa biashara ya mpira. Hivyo klabu zinapoelekea kwenye mabadiliko,
lazima zizingatie hadhi zao zinalindwaje.
Kumi
Chama cha Waandishi wa Habari na Michezo kiliombwa kufanya makongamao
zaidi hasa kuhusiana na aina ya mabadiliko ambayo klabu zinaweza kuingia
kwa sababu inaonekana wanachama ambao ndio wamiliki wa klabu hizi
hawana uelewa wa kutosha hivyo inawapunguzia wigo wa kuchagua aina ya
mabadiliko.
No comments:
Post a Comment