Hii ni taarifa yake kwa vyombo vya habari:
Kituo kwa kupitia dawati la uangalizi wa haki na maboresho kwa mahakama
limekuwa likifuatilia mwenendo wa dhana ya uhuru wa mahakama katika
mgawanyo wa madaraka wa mihimili mitatu ya dola yaani serikali, bunge na
mahakama. Mahakama ni muhimili wa dola ulioundwa na Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania 1977.
Ibara ya 107A (1) inasema kwamba mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji
haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni mahakama. Pia
katika Ibara ya 107B ya Katiba imeipa mahakama mamlaka ya kuwa chombo
huru, ibara hii inasema kwamba katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki,
mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya
katiba na yale ya sheria za nchi.
Ndugu Wanahabari,
Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia mhimili wa serikali ukiingilia
utendaji kazi wa mhimili mwingine wa dola yaani mahakama. Kumekuwepo na
kutolewa na matamko mbalimbali ambayo yanaashiria mhimili wa
utawala/serikali ukiingilia uhuru wa mahakama. Mnamo tarehe 4 Februari,
2016 katika maadhimisho ya siku ya sheria ‘Law Day’ katika hotuba ya
mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliitaka mahakama
kuamua kesi za kodi zipatazo 400 zilizopo mahakamani ambazo alidai
zikiendeshwa ipasavyo basi serikali inaweza kujipatia kiasi cha trilioni
moja. Agizo hili linaonyesha kuwa kesi zote hizo lazima zishinde bila
kujali kuwa mahakama inaongozwa na mambo mengi kufikia uamuzi na hasa
ushahidi ulioko mbele yake.
Pia tumesoma katika gazeti la Mtanzania la tarehe 11 Julai, 2016 Mkuu wa
Wilaya ya Mwanga akidaiwa kumwandikia barua yenye kumbukumbu namba CAB
40/229/01/25 ya tarehe 8 Julai, 2016 Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Mwanga
kutaka taarifa mbalimbali za kesi zinazoendeshwa mahakamani kila mwezi.
Barua hiyo ilitaka taarifa mbalimbali za mahakama zikiwamo idadi ya
kesi zilizopo, zilizosikilizwa na changamoto zilizojitokeza zikiwamo za
sheria, fedha na vitendea kazi kinyume na Ibara ya 107B ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano inayosema katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki,
mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya
Katiba na yale ya sheria za nchi. Agizo hili ni kinyume na Katiba na ni
kuingilia uhuru wa mahakama.
Katika tukio jingine tarehe 12/10/2016 tumeshuhudia mkuu wa wilaya ya
Kinondoni akimwamuru mwenyekiti wa baraza la ardhi la wilaya Kinondoni
kwamba shauri no 331/2014 lisikilizwe upya baada ya mlalamikaji katika
shauri hilo kutoridhishwa na maamuzi ya baraza la ardhi la wilaya. Iwapo
mlalamikaji hakuridhika na uamuzi wa mahakama anapaswa kukata rufaa au
kufuata taratibu nyingine za kumahakama na si mtawala wa seriakali kutoa
maagiza kwa mahakama.
Ndugu Wanahabari,
Kituo cha sheria na haki za binadamu kinatoa mapendekezo yafuatayo.
i. Mhimili wa serikali katika kutekeleza majukumu yake izingatie sheria
na katiba ya nchi na kusiwepo na kuingilia uhuru wa mahakama kama
ilivyoanishwa katika Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
ii. Serikali, Bunge na Mahakama kuheshimu na kuzingatia dhana ya
mgawanyo wa madaraka na pasiwepo mhimili mmoja kuingilia mhimili
mwingine.
iii. Ibara ya 107A ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977
imeipa mahakama mamlaka ya mwisho ya utoaji haki hivyo kusiwepo na
chombo chochote kitakachoingilia kazi ya mahakama. Masual ya kimahakama
yafuatiliwe kimahakama na si vinginevyo
iv. Tungetegemea Jaji Mkuu kutoa muongozo na kuzungumazana na seriakali
katika suala hili ili kuweka msimamo katika misingi ya kisheria na
kikatiba.
Imetolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji.
No comments:
Post a Comment