Waziri wa ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya makazi Mhe. William Lukuvi akionesha nyaraka zilizoghushiwa
na mmoja wa raia wa kigeni Bw. Hamant Patel alizotumia kujipatia fursa
ya kumiliki ardhi kama raia.
Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Katika siku za hivi karibuni
kumetokea wimbi kubwa la matapeli wanaotumia nyaraka za kughushi
zinazodaiwa kuwa ni Barua za Toleo zilizotolewa na iliyokuwa ofisi ya
ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam. Nyaraka hizo za kughushi
zimesababisha wananchi kupoteza fedha na mali na kuongezeka kwa migogoro
mingi ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dare es salaam.
Napenda kuwatahadharisha
watendaji na umma wote kwa ujumla kuwa waangalifu wakati wa kuingia
kwenye miamala ya mauziano au utayarishaji wa hati milki kwa kutumia
nyaraka za aina hiyo. Hivyo kuanzia sasa kusifanyike muamala wala
utayarishaji wa hati yoyote kwa kutumia nyaraka za aina hiyo mpaka ziwe
zimehakikikwa na Kamishna wa Ardhi. Aidha, kwa wananchi wanaojihusisha
na utumiaji au utayarishaji wa nyaraka za kughushi watambue kuwa hilo ni
kosa kisheria na watakaobainika Wizara itahakikisha sheria inachukua
mkondo wake.
Ninaagiza wananchi wote wenye
nyaraka halali zilizotolewa na iliyokuwa Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri
ya Jiji la Dar es salaam, wazirejesha kwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi.
Ofisi hiyo itaweka mpango maalumu wa kuhakiki na kutoa Hati Milki.
Atakaye leta nyaraka za kughushi atakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo
vya dola.
B: UVAMIZI WA MAENEO YA UMMA, MASHAMBA NA VIWANJA VYENYE HATI MILKI
Nimepokea taarifa za kuwepo kwa
uvamizi mkubwa wa mashamba na viwanja vinavyomilikiwa kisheria. Uvamizi
huo unafanywa kwa vizingizio mbalimnbali ikiwemo wavamizi kudai kuwa ni
mapori, uhaba wa ardhi na sababu nyinginezo zisizo za kisheria. Kuvamia
shamba au kiwanja ni kosa la jinai kwa mujibu wa fungu la 175 la Sheria
ya Ardhi Na. 4 (1999).
Ninazo taarifa pia za uvamizi
mkubwa katika maeneo ya Mabwepande, Pugu Kajiungeni na maeneo ya
Bagamoyo na maeneo mengine nchini. Ninazo taarifa pia baadhi ya viongozi
wanashiriki katika kusaidia uvamizi wa viwanja na mashamba ya watu. Na
wavamizi hawa wamethubutu hata kuwatisha maofisa wetu wanapokuwa kazini.
Tabia hii haiwezi kuvumiliwa na lazima hatua kali za kisheria
zichukuliwe. Sheria inaweka wajibu wa msingi kwa vyombo vya dola,
Halmashauri na wamiliki kulinda haki za kumiliki ardhi.
Ninamwagiza Kamishna wa Ardhi, na
Makamishna Wasaidiziwa Kanda kuweka mkakati maalum wa kukomesha tabia
hiyo ya uvamizi kwa kushirikiana na vyombo vya dola na ofisi za
Halmashauri.
C: UDANGANYIFU WA URAIA KWA AJILI YA KUJIPATIA MILIKI ZA ARDHI
Sheria za ardhi zinaelekeza kuwa
ardhi ya Tanzania itamilikishwa kwa raia wa Tanzania. Wageni wanayo
fursa ya kupata ardhi hiyo ikiwa wataihitaji kwa ajili ya uwekezaji
kupitia Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC). Tunazotaarifa kuwa baadhi ya
wageni (foreigners) wakishirikiana na raia hufanya udanganyifu na
kughushi nyaraka za uraia ili kujipatia miliki za ardhi kama raia.
Udanganyifu huo umekuwa pia ukifanywa na makampuni ambayo hujisajili
kama makampuni raia kwa kutoa hisa nyingi kwa raia na mara baada ya
kupata ardhi huhamisha hisa zote kwenda kwa wageni.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.
4 (1999) Kampuni ni raia iwapo tu hisa nyingi (majority shares) katika
kampuni hiyo zinamilikiwa na raia. Inapotokea mabadiliko ya umiliki wa
hisa kwenye kampuni kupelekea hisa nyingi kumilikiwa na wageni, Kampuni
hiyo inakoma kuwa raia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 (1999) na
inakosa sifa ya kumiliki ardhi kama raia tangu siku ambayo itasomeka
hisa nyingi zinamilikiwa na wageni.
Tumeanza sasa kazi ya kuhakiki
kwa kushirikiana na Msajili ya Makampuni (BRELA) makampuni yote
yanayomiliki ardhi kama raia ili kubaini kama bado yana sifa ya kumili
ardhi kama raia. Na iwapo itabainika kuwa kampuni imepoteza sifa ya
uraia, hatua za kisheria zitachukuliwa juu ya miliki ya ardhi
inayomilikiwa na Kampuni hiyo ikiwemo kurejesha ardhi hiyo mikononi mwa
serikali.
Kwa wageni ambao wameghushi
nyaraka za uraia na kujipatia fursa ya kumiliki ardhi kama raia,
tumeweka mkakati maalum kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kuwabaini
na mara ikithibitika tutafuta miliki zao.
Nawatakia Siku Njema
William Vangimembe Lukuvi (Mb)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
No comments:
Post a Comment