Wednesday, 19 October 2016

khalfan-ngasa-babu
Kocha Khalfan Ngassa amekuwa kwenye benchi la timu ya mpira wa miguu ya Toto Africans ya Mwanza akiwa kocha msaidizi kwa mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Khalfan Ngassa aliongoza timu kwenye mchezo Na. 62 dhidi ya Kagera Sugar Oktoba 7, 2016; mchezo Na. 67 dhidi ya Mbao FC uliofanyika Oktoba 12, 2016 na Mchezo Na. 79 dhidi ya Majimaji ya Songea uliofanyika Oktoba 15, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 72 (3) (5) ya Ligi Kuu, Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja B ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) na Daraja C kwa Kocha Msaidizi pia kutoka CAF.
Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limethibitisha kuwa Kocha Khalfan Ngassa  hana leseni yoyote kati ya hizo, hivyo hastahili kukaa kwenye benchi la timu ya Toto Africans kama kocha mkuu au kocha msaidizi.
Kitendo kinachofanywa na Toto Africans ni ukikwaji wa kanuni na ni vema uongozi wa Toto ukamwondoa Khalfan Ngassa kwenye benchi ili kuepuka adhabu. Kipendele cha (7) cha kanuni hiyo ya 72, inaelekeza adhabu kuwa inaweza kutozwa si chini ya Sh 500,000 (shilingi laki tano).
Pia tunazikumbusha klabu zote kuwa kuanzia msimu ujao wa 2017/18 wa Ligi Kuu ya Vodacom, kocha anayestahili kukaa kwenye benchi ni yule mwenye leseni Daraja A kwa nafasi ya Kocha Mkuu na angalau Leseni Daraja B kwa kocha msaidizi..

No comments:

Post a Comment