Sunday, 30 October 2016

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Taasisi ya Twaweza wameunga mkono Mswada wa Huduma za Habari ya mwaka 2016

twaweza
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Taasisi ya Twaweza wamesema kuwa Muswaada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ni bora kuliko Miswada iliyowahi kuwasilishwa nchini.
Haya yamebainishwa katika maoni yao waliyowasilisha kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Mjini Dodoma katika juhudi za kuufanya Muswada huo kuwa bora zaidi na kupelekea kuapa sheria yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
TLS na Twaweza wamebainisha kuwa Muswada huu ni bora zaidi  na utasaidia kuwajengea wadau wa habari nchini heshima kwa kutoa huduma bora kupitia  vyombo vya habari kwa kuzingatia taaluma ya Habari waliyonayo hatua ambayo inautofautisha na muswada uliowasilishwa Bungeni mwaka 2015.
Kwa mujibu wa maoni yalitolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) yamesema Muswada huo mzuri zaidi na unaifuta Sheria ya  Magazeti ya Mwaka 1976 hatua ambayo wameipongeza Serikali kwani Sheria hiyo  iliwahi kuainishwa kuwa miongoni mwa Sheria 40 na kusadikiwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali kama Sheria kandamizi.
Kwa upande wa Taasisi ya Twaweza wao wamesema kuwa Muswada huo utaanzisha utaratibu ambao utawatambua waandishi wa habari kwa kuanzisha Baraza Huru la Habari pamoja na Bodi ya Ithibati ya wanahabari amabazo zitasimamia kanuni na maadili ya wanahabari, kusimamia viwango na mienendo ya kitaaluma na kuendeleza vigezo bora vya maadili na nidhamu miongoni mwa wanahabari.
Kwa mantiki hiyo, maoni yaliyowasilishwa kwa Kamati hiyo yanaendana na Muswada ambao unasisitiza  kuanzisha mahusiano na taasisi nyingine za taaluma ya habari ndani na nje ya nchi ili wadau wa habari waweze kubadilishana mawazo na kuwa na namna bora ya kuhabarisha umma katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, Baraza huru la habari kutakuwa suluhisho katika kusimamia na kusikiliza malalamiko ambayo yatawasilishwa kwenye baraza hilo kulingana na kanuni za maadili ya taaluma ya habari hatimaye kuifanya tasnia ya habari kuheshimika tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.
Uboreshwaji wa Muswada huo unalenga kuleta Sheria itakayosimamia Tasnia ya Habari ili iweze kuendana na wakati pamoja na Sheria za kimataifa na namna bora ya kuwahudumia wananchi.

No comments:

Post a Comment