Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiongozana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa
Rwekaza Mukandala (kulia kwake) kuelekea kwenye ukumbi wa Nkurumah
baada ya kuwasili kwenye Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuhutubia kwenye
kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho Oktoba 25, 2016. Kulia
ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ally Happy, kushoto ni Rais wa Jumuiya ya
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Jaji Joseph Warioba na wapili
kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinoloji,
Dkt. Leonard Akwilapo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwa na makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Rwekaza
Mukandala baada ya kwasili kwenye ukumbi wa Nkurumah chuoni hapo
kuhutubia kwenye kilelele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho
Oktoba 25, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akihutubia kwenye kilele cha Maadhiisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha
Dar es salaam kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba 25,
2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akionyesha Kitabu Kiitwacho From Lumumba Street to the Hill and
Beyond baada ya kukizindua katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya
Chuo Kikuu cha Dar es salaa baada ya kuhutubia kwenye ukumbi wa Nkurumah
jijini Dar es salaam. Katikati ni Makamu Mkuu wa CHuo Kikuu cha Dar es
salaam, Profesa Rwekaza Mukanda na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt Leonard Akwilapo. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizindua Kitabu Kiitwacho From Lumumba Street to the Hill and Beyond
katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es
salaa baada ya kuhutubia kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam
Oktoba 25, 2016. Katikati ni Makamu Mkuu wa CHuo Kikuu cha Dar es
salaam, Profesa Rwekaza Mukandala na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt Leonard Akwilapo. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiteta na Rais wa Jumuiya wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam,
Jaji Joseph Warioba baada ya kuhutubia kwenye kilele cha Maadhimisho ya
Miaka 55 ya chuo hicho kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam
Oktoba 25, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam wa zamani,
Balozi Nicholas Kuhanga baada ya kuhutubia kwenye Maadhimisho ya Miaka
55 ya Chuo hicho kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba
25, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dae es salaam wa zamani
Profesa Matthew Luhanga baada ya kuhutubia kwenye kilele cha
Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini
Dar es salaam Oktoba 25, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya waliohudhuria kwenye
kilele cha Maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam
wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye
ukmbi wa Nkuruma jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
*Waziri Mkuu ataka vyuo viweke utaratibu bayana wa kurithishana kazi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedhaza mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba
pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa lakini pia amevitaka
vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi
(succession plan).
Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na
masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na
maprofesa kuwa miaka 70.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga
kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K.
Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa
wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa
taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu
nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba
kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.
Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za
kutosha kwa ajili ya mafunzo,” amesema.
“Lakini vyuo vya elimu navyo havina budi kuweka taratibu na mipango
endelevu ya kurithishana (kuachiana nafasi) ‘Succession Plan’. Jambo
hii ni muhimu sana kwani bila hivyo, wakati wote kutakuwa na pengo
kubwa katika utoaji wa taaluma,” amesisitiza.
Amesema Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa
mipango hii ya kuwa na watalaamu wa kutosha katika vyuo huku
ikiendelea kutekeleza majukumu ya kuwaajiri wanataaluma na wafanyakazi
wapya pale wanapohitajika.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi
wote wa umma na hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za
kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa.
“Hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2016 zoezi linaloendelea hivi sasa,
limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500. Baada ya
zoezi hilo, tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa
Serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote,” amesema.
“Ninafahamu kuwa yapo madai mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya
mishahara kwa watumishi hususan baada ya kuanza kwa muundo wa pamoja
wa wanataaluma wa vyuo vikuu vya umma. Serikali inaendelea na
maboresho na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia
bodi ya mishahara na motisha; na mara tutakapokamilisha, tutapanga
upya mishahara na motisha kwa watumishi,” amesema.
Akifafanua kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu
amesema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa
mikopo. Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo
wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ilikwishaongeza bajeti ya
mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi sh.
bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017.
Mapema, akielezea utendaji kazi wa chuo hicho katika miaka yote 55,
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala amesema chuo hicho
kinakabliwa na changamoto ya uhaba wa wanataaluma waandamizi wa fani
mbalimbali.
“Chimbuko la changamoto hii ni kusitishwa kwa ajira katika taasisi za
umma kwenye miaka ya 1990. Kutoajiriwa kwa wanataaluma chipukizi kwa
miaka mingi, kulivuruga utaratibu wa miaka mingi wa kurithishana
uzoefu baina ya wanataaluma wanaostaafu na wale ambao wangelichukua
nafasi zao,” amesema.
“Hali hii iko kwenye vyuo vikongwe ambako mamia ya wanataaluma wazoefu
wanastaafu kwa wakati mmoja na wengi wa wanataaluma walioajiriwa hivi
karibuni bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na
hivyo hawana uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha katika
ngazi za digrii za umahiri na uzamivu,” amesema.
Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kuwadhamini
wahadhiri chipukizi ambao wako sehemu mbalimbali wakipata mafunzo. Pia
amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga
hosteli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,800 na hivyo
kutarajiwa kupunguza tatizo la malazi.
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga kiasi
cha sh. bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye
chuo hicho zikiwemo maabara.
No comments:
Post a Comment