Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi
Evarist Ndikilo akizungumza jambo kuhusiana na uzinduzi wa maonyesho ya
tisa(9) ya wajasiriamali mwaka 2016 yanayotarajiwa kufanyika wilayani
Bagamoyo.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WAJASIRIAMALI hasa
wadogowadogo wametakiwa kuchangamkia fursa ya kutangaza na kutafuta soko
la bidhaa zao katika maonyesho ya tisa (9)ya wajasiriamali mwaka 2016,
yanayotarajiwa kufanyika wilaya ya Bagamoyo kuanzia octoba 26 hadi 31
mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Pwani
mhandisi Evarist Ndikilo, alitoa rai hiyo wakati akizungumza na
waandishi wa habari kufuatia mkoa huo kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa
maonyesho hayo yanayoratibiwa na sido Kanda ya Mashariki.
Katika maonyesho hayo
wajasiriamali zaidi ya 280 kutoka mikoa ya kanda hiyo ikiwemo Pwani,
Morogoro, Lindi, Dar es salaam na Mtwara wanategemewa kushiriki.
Alisema shughuli hiyo itafanyika katika uwanja wa CCM, Mwanakalenge karibu na chuo cha sanaa, Bagamoyo (TASUBA).
Aidha alieleza mgeni
rasmi wakati wa uzinduzi wa maonyesho anatarajiwa kuwa waziri wa
viwanda, biashara na uwekezaji, Charles Mwijage (mb).
“Kauli mbiu ya maonyesho
ya mwaka huu ni uchumi wa viwanda unategemea viwanda vidogo ambapo
maadhimisho ya maonyesho haya nitafunga mimi mkuu wa mkoa “alifafanua
mkuu huyo wa mkoa.
Mhandisi Ndikilo alisema
endapo fursa hiyo itatumika ipasavyo itasaidia wajasiriamali hususan wa
vijijin lakini na wa mjini kutangaza bidhaa zao.
Hata hivyo alielezea
kuwa maonyesho hayo yatawawezesha kuwakutanisha wazalishaji wa bidhaa
mbalimbali ili waweze kubadilishana uzoefu wa kiufundi, masoko na ubora
wa bidhaa.
Mhandisi Ndikilo
alisema wafanyabiashara hao watakuza ubora wa bidhaa, kupata mbinu za
ushindani, kuwajengea uwezo wajasiriamali kujiamini na kuona wanaweza
kuuza bidhaa.
Madhumuni mengine ni
kupata mafunzo yanayoandaliwa na sido kabla ya maonyesho na maandalizi
kwa ajili ya soko la Afrika mashariki na utandawazi.
Mhandisi Ndikilo,
alifafanua kuwa wananchi na viongozi pia wataweza kuona bidhaa
zinazozalishwa na kutambua uwezo wa wajasiriamali husika.
Alisema wilaya ya
Bagamoyo ni wilaya ya kiutalii, ipo shwariiii na hatua stahiki za
kiusalama zitachukuliwa ili kuhakikisha wageni na wajasiriamali wanakuwa
salama.
Meneja wa sido mkoani
Pwani, Agnes Yesaya alitaja bidhaa zinazotarajiwa kuonyeshwa ni pamoja
na mashine mbalimbali za uzalishaji bidhaa zilizosindikwa.
Bidhaa nyingine ni zile
zinazotokana na kazi mbalimbali za mikono, sabuni, bidhaa za ngozi,
bidhaa mchanganyiko zinazotoka kwenye mikoa na kanda nyingine.
Agnes alisema taasisi za
serikali na binafsi ikiwemo shirika la viwango (TBS), bodi ya biashara
za nje (BET)nazo zitakuwepo kwa ajili ya uhamasishaji wa wajasiriamali
kuhusu viwango na ubora na namna ya kuuza bidhaa nje ya nchi.
Serikali mkoa wa Pwani
na sido mkoa, walitoa wito kwa pamoja kuiomba jamii na wadau wa
kibiashara kujitokeza kufika Bagamoyo kuona na kununua bidhaa
zinazozalishwa ndani ya nchi.
“Watanzania wabadilike kwa kupigania na kununua bidhaa zinazotokana na ubunifu na mikono ya watanzania wenzao”walisema.
Mhandisi Ndikilo na
meneja wa Sido mkoa wanasema ni faraja kununua bidhaa za nchini kwani
hazinatofauti na zile za nje ya nchi na zinauzwa kwa gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment