Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na WatotoMh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi
wa habari wakati alipokuwa akitoa tamko la serikali kuhusu Takwimu za
viashiria vya Ukimwi na Maralia mwaka 2011-2012 na kiwango cha
maambukizi ya Ukimwi (VVU) kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi.
Kwa mujibu wa Takwimu za
Viashiria vya UKIMWI na Malaria za mwaka 2011-2012, kiwango cha
maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) nchini kinakadiriwa kuwa ni
asilimia 5.1 miongoni mwa watu wazima wenye umri kati ya miaka 15 – 49.
Takwimu hizi zinaashiria kwamba, kwa kila watanzania 1000, watu 51
miongoni mwao wanaoishi na maambukizi ya VVU. Inakadiriwa kuwa, kuna
watu 1,400,000 wanaishi na VVU nchini Tanzania ambapo, watu 839,574
wanapatiwa tiba ya dawa za kupunguza makali ya VVU zinazotolewa katika
vituo 4,000 vilikuwa vinatoa huduma hiyo nchi nzima hadi kufikia mwezi
Juni mwaka huu (2016).
Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wadau wake imechukua hatua za
makusudi na za haraka katika kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI na UKIMWI. Serikali imefanikiwa kuanzisha na kutekeleza mipango
mbalimbali ya kuzuia maambukizi mapya kwa kutoa huduma za kinga, tiba na
matunzo kwa walioambukizwa VVU katika ngazi ya vituo vya huduma za afya
na ngazi ya jamii. Mikakati yote hii imelenga kuboresha afya kwa
kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kutokomeza kabisa UKIMWI.
Mbali na Mipango mikakati na
mbinu madhubuti ambazo zimetekelezwa bado takwimu zinaonesha kuwa
kiwango cha maambukizi miongoni mwa makundi maalum na yale yaliyo katika
hatari zaidi ya kuambukizwa VVU yapo juu kulinganisha na kiwango
kilichopo kwa jamii kwa ujumla.
Kutokana na mazingira yetu
makundi maalum ni makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukiza na
kuambukizwa VVU, kwa kuzingatia takwimu za maambukizi ya VVU kwa makundi
haya kuwa juu, Serikali imeainisha makundi haya kama ifuatavyo:-
Wasichana walio katika umri wa
balehe walio katika mazingira hatarishi, vijana walio katika umri wa
balehe, watoto yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi (yaani
watoto wanaoishi mitaani), wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao,
wanawake wanaofanya ngono kinyume na maumbile, watu wanaotumia dawa za
kulevya hasa wale wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga
sindano, wanawake wanaofanya biashara ya ngono na wateja wao, wafungwa,
wakimbizi na wafanyakazi wanao hamahama hasa madereva wa malori ya
masafa marefu, wachimba madini na jamii zilizopo katika maeneo ya
migodi, wavuvi na jamii zilizopo katika maeneo ya uvuvi, wafanyakazi wa
kwenye mashamba makubwa, wajenzi wa barabara na watu wenye ulemevu.
Kuna ushahidi wa kipiedemilojia
kwa programu za VVU na UKIMWI kulenga makundi maalum. Katika nchi
zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, vijana balehe wenye umri wa
miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 35 ya maambukizi mapya ya VVU.
Aidha, kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU nchini Tanzania,
kinaonekana miongoni mwa makundi maalum (asilimia 26 miongoni mwa
Wanawake wanaofanya Biashara ya Ngono, asilimia 36 miongoni mwa
wajidunga na asilimia 25 miongoni mwa wanaume wanaofanya ngono na
wanaume wenzao).
Serikali ya Tanzania kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilianza
kutoa huduma za VVU na UKIMWI kwa makundi maalum na yale yaliyo katika
hatari zaidi ya kuambukizwa na kuambukiza VVU tangu mwaka 2010 baada ya
kufanya tafiti na kugundua kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kiko juu
ikilinganishwa na makundi mengine kwenye jamii. Huduma hizi zimekuwa
zinatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya Jamii
katika Mikoa mbalimbali nchini.
Hivi karibuni kumekuwepo na
taarifa kuwa Asasi za Kiraia (za hapa nchini na za Kimataifa) zimekuwa
zinapitia katika Afua ya kupambana na UKIMWI ili kuhamasisha mapenzi ya
jinsia moja, na hii imepelekea Waziri wa Katiba na Sheria kutamka
kupitia vyombo vya habari kuwa atavichukulia hatua za kisheria asasi
hizo ambazo zinakiuka taratibu na sheria zilizowekwa na Serikali.
Napenda kutamka kwamba, Wizara
yangu halitalifumbia macho suala hili, na napenda kuziasa asasi zote za
kiraia za ndani na nje ya nchi kufanya kazi kwa kufuata taratibu na
sheria za nchi na kutoa afua zenye lengo la kupambana na maambukizi
mapya ya VVU katika makundi haya na jamii kwa ujumla. Aidha nazitaka
asasi hizo kutoa huduma bora zenye kiwango cha kimataifa lakini pia
huduma zinaoendana na utamaduni, mila na desturi za Mtanzania huku
zikizingatia sheria za nchi kama vile sheria ya kanuni ya adhabu, sura
ya 16 kama ilivyofanyiwa marakebisho mwaka 2002.
Tukumbuke kwamba Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina
jukumu la kutoa huduma za Afya na zile za kupambana na UKIMWI bila
ubaguzi, na vilevile bila kujali jinsi, kabila, dini, hali ya kifedha,
rangi au chama cha mtu yeyote.
Baada ya kubaini changamoto
katika utoaji wa huduma za Afya na zile za kupambana na UKIMWI kwa asasi
zisizo za Serikali, niliitisha kikao na wadau wa maendeleo wanao
fadhili na kutoa huduma za kupambana na UKIMWI katika makundi haya
maalum ili niweze kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa ya msingi ikiwemo
kuweka bayana suala la kutoa huduma za VVU kwa makundi haya huku
tukizingatia taratibu na sheria za nchi (Public Health Approach to HIV
programming to PK).
Yafuatayo ni matamko niliyoyatoa na ambayo wote tunapaswa kuyazingatia:
Serikali itaendelea kutoa
huduma za Afya na zile za kupambana na UKIMWI bila ubaguzi wa jinsi,
kabila, dini, hali ya kifedha, rangi au chama cha mtu yeyote.
Kwa kuwa maambukizi ya VVU kwa
makundi maalum bado yapo juu ukilinganisha na jamii kwa ujumla, Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, JInsia, Wazee na Watoto
itaendelea kutoa kitita cha huduma kama kitakavyopitiwa na kuainishwa na
miongozo ya kutolea huduma za kupambana na UKIMWI katika makundi
maalum.
Makundi Maalum kwa mantiki ya
Tanzania itabaki kuwa ya kiujumla kama yalivyo tajwa hapo juu ambayo
yanaendana na mazingira ya Tanzania, hivyo maana na tafsiri hiyo ifuatwe
na kuzingatiwa katika huduma au afua zinazotekelezwa na wadau wote
wanao shirikiana na Serikali katika kutoa huduma za VVU na UKIMWI
nchini.
Kila mdau wakati wote atoe
huduma kwa mujibu na sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inayotaka mtu kuchukuliwa sheria
endapo atathibitika kufanya mapenzi na mtu wa jinsia moja., na kama mdau
ni shirika lisilo la Serikali pia ana wajibu wa kuzingatia Sheria Na 24
ya Mwaka 2002 ya Asasi zisizo za Kiserikali, na kufuata maadili ya kazi
za NGO (NGO code of conduct).
Huduma za Makundi maalum na
yale yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa na kuambukiza VVU
zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya zitaendelea kwa
makundi yote isipokuwa huduma za ngazi ya jamii kwa wanaume wanaofanya
ngono na wanaume wenzao, hizi zitasubiri mwongozo mpya wa utoaji wa
huduma ngazi ya jamii. Huduma mkoba zinazotolewa na watoa huduma za
afya toka vituoni zitaendelea kutolewa kwa mujibu wa miongozo iliyopo.
Wizara inaweka msisitizo mkubwa katika kuunganisha huduma zinazofanana
na utoaji wa rufaa katika vituo vya huduma za afya kwa mwendelezo wa
huduma. Taratibu za utekelezaji zitafafanuliwa na Wizara ndani ya wiki
moja.
Kutokana na kuongezeka kwa
idadi ya wadau wanaotaka kushirikiana na kuisaidia Serikali katika kutoa
huduma hizi, hasa kwa kuzingatia tabia ya kuhama hama kwa makundi haya
kutoka eneo moja hadi jingine, kumekuwa na mwingiliano wa huduma
zinazotolewa kwa makundi haya, mwingiliao huu unahatarisha ubora wa
huduma. Ili kuleta tija, uwajibikaji na uwazi, Mganga Mkuu wa Serikali
ataongoza zoezi la kupanga upya wadau katika Mikoa watakayotoa huduma
kwa nchi nzima.
Asasi zote za kiraia za hapa
nchini zinazotekeleza afua za VVU na UKIMWI katika Halmashauri lazima
ziidhinishwe na Halmashauri husika kabla hazijaruhusiwa kufanya kazi na
asasi zisizo za kiserikali za kimataifa. Kwa maneno mengine, Asasi
zisizo za kiserikali za kimataifa zitapewa orodha ya asasi za kiraia
zilizoidhinishwa kufanya kazi katika Halmashauri au Wilaya husika.
Kanuni za Msingi za Ushirikiano (MOU) zitaandaliwa kati ya wadau watatu,
yaani Asasi ya Kimataifa, Asasi ya Kiraia ya hapa nchini na Halmashauri
au Wilaya husika. Nakala ya Kanuni za Msingi za Ushirikiano (MOU)
ziwasilishwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
(Idara ya Maendeleo ya Jamii) na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI.
Wakati huohuo, mkakati wa
usambazaji wa vilainishi hauruhusiwi kutolewa kama afua mojawapo ya
kuzuia VVU kwa sasa. Serikali inahitaji muda wa kutosha wa kujiridhisha
kuhusu umuhimu wa matumizi yake kama kinga ya kuzuia VVU na pia kuhusu
kukubalika katika jamii yetu. Endapo Serikali itaridhia jambo hili, basi
hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango ya
manunuzi na usambazaji wake ikitumia mfumo ya kusambaza vifaa tiba.
No comments:
Post a Comment