Monday, 24 October 2016

Mtu mmoja amekufa na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali ya basi Songea.

Mtu mmoja amepoteza maisha na majeruhi kumi na nane kufuatia ajali ya basi la abiria la kampuni ya Superfeo,na kwamba ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Gumbilo wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,ambapo baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wameelezea chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa barabara ambayo imefanyiwa ukarabati siku za hivi karibuni.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma,Zuberi Mwombeji amelitaja gari hilo kuwa ni namba T.431 DBV ambalo linafanya safari zake kutoka jijini Mbeya kwenda wilaya ya Mbinga mkoani hapa ambapo mara baada ya kutokea ajali hiyo mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Binilith Mahenge alienda eneo lililotokea ajali na baaadae  aliwajulia hali majeruhi waliokuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Nae Mganga wa zamu hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma Dk.Yohana Mwakabumbe amekiri kupokea mwili mmoja wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Kanisius Mvula mkazi wa Peramiho mwenye umri wa miaka 20na majeruhi kumi na nane ambapo majeruhi sita wamelazwa hospitalini hapo na wengine wametibiwa na kuruhusiwa na kwamba hali za majeruhi zinaendelea vizuri.
Kwa upande wao majeruhi wa ajali hiyo wamesema kuwa mwendo wa gari hilo ulikuwa ni wa kawaida na kuongeza kuwa mikanda waliyojifunga ndiyo iliwasaidia kutopata madhara zaidi na hapa wanafafanua.
Ikiwa umepita mwezi mmoja sasa ambapo wananchi mkoani hapa wakiwa bado na majonzi kufuatia ajali nyingine iliyotokea katika kijiji cha Lilombwi wilayani Njombe na kusababisha vifo vya watu kumi na wawili,baadhi ya wananchi mkoani hapa wamelitaka jeshi la polisi kuwadhibiti madereva wasiozingatia sheria za usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment