Na Shamimu Nyaki WHUSM.
Serikali imesema kuwa Muswada wa
Sheria ya Huduma ya Habari unatoa fursa kwa wanahabari mbalimbali kuwa
na Haki ya kupata Bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji wa Serikali Bw. Hassan Abbas
alipokuwa akizungumza katika kituo cha Redio E Fm kilichopo Jijini Dar
es Salaam, ambapo ameeleza kuwa Muswada huu utatoa fursa kwa wanahabari
kupata Bima ya Afya na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa fedha ya
matibabu .
“Muswada huu utasaidia
wanahabari kuwa na Bima ya Afya itakayosaidia kupata huduma ya kiafya
na kuacha utaratibu ulipo sasa wa kutoa michango wakati mwanahabari
anapokuwa mgonjwa au anapofariki.” Alisema Bw. Abbas.
Aidha Mkurugenzi huyo ameongeza
kuwa Sehemu ya tatu ya Muswada huu unaeleza kuwa kutakuwa na Mfuko kwa
ajili ya Habari ambao lengo lake kuu ni kuwezesha mafunzo kwa
wanataaluma ya habari pamoja na kukuza na kuendeleza utafiti na
maendeleo katika nyanja ya Habari na Mawasiliano ya Umma.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi
huyo ametoa rai kwa wadau na wanatasnia kwa ujumla kuusoma Muswada huu
na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kuuboresha ili uweze kutumika kwa
ajili ya maendeleo ya Tasnia ya Habari.
“Naomba wadau muusome Muswada huu
muuelewe na muweze kutoa maoni yenu kabla haujapelekwa Bungeni kwa mara
ya pili ili tasnia hii iwe na hadhi kama inavyostahili.” Aliongeza Bw
Abbas.
Muswada wa Sheria ya Huduma za
Habari ya mwaka 2016 upo katika hatua ya kujadiliwa na Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na wadau kutoa maoni kwa ajili
ya kuuboresha Muswada huo kabla ya kuwasilishwa Bungeni kujadiliwa.
No comments:
Post a Comment