Anitha Jonas – MAELEZO
Wahariri wa vyombo vya habari
wameukubali Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari baada ya kuusoma kwa
umakini nakuona namna gani utasaidia kuinua tasnia ya habari nchini.
Hayo yamebainishwa katika
mahojiano maalum kwa njia ya simu na baadhi ya wahariri wa vyombo vya
habari akiwemo Mhariri wa Televisheni ya TV 1, Bw.Said Mwishehe huku
akieleza faida za Muswada huo pamoja na kutoa maoni yake kwa kuiomba
serikali kuangalia vizuri baadhi ya vipengele na kama kipengele cha 54
na 55 katika Sehemu ya Nane ili kuvipunguzia makali na kuondoa suala la
kuonekana kubana uhuru wa vyombo vya habari.
“Kuna umuhimu kwa wadau wa habari
kuunga mkono muswada huu badala ya kuupinga kwani una mambo mazuri
yatakayosaidia kuboresha tasnia hii ya habari na kuipa heshima kama
taaluma nyingine badala ya kuonekana kuwa waandishi wa habari ni watu
wababaishaji tu na wasiyo na taaluma iliyo imara,”alisema Bw.Mwishehe.
Pamoja na hayo Mhariri huyo
aliendelea kusema amefurahishwa na muswada kwa namna unavyojali maslahi
ya waandishi wa habari pale unapoeleza kuwa wamiliki wa vyombo vya
habari watahitajika kuwakatia bima waandishi wa habari kwa hiyo itakuwa
jambo la busara kwani waandishi wamekuwa wakifanya kazi katika
mazingira magumu yanayohatarisha afya zao pasipo kuwa na bima
inayomlinda akiwa kazini.
Aidha, Bw.Mwishehe aliwasihi
wadau wa sekta ya habari kutuma maoni yao kwa vile vipengele vya muswada
vinavyoonyesha kutokuwa sawa na pia ameiomba serikali kuwa na utayari
wa kuyapokea maoni hayo kwa ajjili ya kuboresha muswada huo na kuufanya
bora na wenye tija katika tasnia ya habari nchini.
Naye Mhariri wa Gazeti la
Mtanzania, Bw.Revocatus Makaranga alisema Muswada huo wa habari una
mambo mazuri yanayoipeleka tasnia mahali pazuri ikiwemo suala la
waandishi wa habari kuhitajika kujiendeleza katika elimu ya juu na hii
itasaidia kukuza upeo wa mwandishi na kumfanya awe na uwezo mkubwa na
kufanya kazi kwa kujiamini kama ilivyo kwa waandishi wa nchi
zilizoendelea.
Bw.Makaranga aliongeza kusema
muswada una vipengele ambavyo ipo haja ya serikali kuvifanyia
marekebisho ikiwemo suala la adhabu inayotolewa kwa waandishi ya
kuwafungia pale wanapokuwa wamekosea.
Pia mhariri huyo ameipongeza
serikali kwa muswada huo ambao utaleta picha mpya ya kimaendeleo katika
tasnia ya habari ikiwemo suala la kuanzishwa kwa Mfuko wa mafunzo kwa
wanahabari nchini ambapo utasaidia kutoa elimu kwa waandishi mara kwa
mara na kuwajengea uwezo wa utendaji.
Kwa upande wake, Mhariri Mkuu wa
kituo cha Redio Efm, Bi Scolastika Mazula alisema katika muswada huo wa
habari yapo mambo mazuri yenye tija katika sekta ya habari kama suala la
kuanzishwa kwa Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari ni jambo jema sana kwani
utasaidia kutoa fursa za waandishi kujiendeleza kimasomo na kuifanya
fani ya habari kuwa na wasomi zaidi tofauti na inavyoonekana kwa sasa.
“Suala la elimu kwa waandishi ni
bora liwekwe wazi kisheria kwani tansnia hii ya habari inahitajika
kuheshimika kama ilivyo tansia nyingine badala ya kuonekana
wababaishaji”, alisema Mazula.
Pamoja na hayo Bi. Mazula
aliendelea kutoa maoni yake kuhusu Muswada kwa kusema kuwa suala la
kuanzishwa kwa bodi ni zuri ila ingekuwa vyema kama bodi hiyo itakuwa na
asilimia kubwa ya wadau wa habari na ijitegemee na Waziri mwenye
dhamana ya habari na Mwanasheria Mkuu wasiwe na mamlaka sana katika bodi
hiyo.
Pamoja na hayo naye Katibu wa
Jukwaa la Wahariri, Bw.Neville Meena alisema kwa sasa wanajukwaa
wameshatoa maoni yao kuhusu muswada huo na watayawasilisha kwa ajili ya
kusaidia kuboresha muswada huo na kuufanya uwe na tija na manufaa zaidi
katika kuendeleza tasnia ya habari nchini.
No comments:
Post a Comment