Thursday, 27 October 2016

Baharia atoweka akijaribu kuvunja rekodi ya dunia

Guo Chuan ndiye baharia anayefahamika zaidi kutoka Uchina
Baharia mashuhuri kutoka China Guo Chuan ametoweka akijaribu kuvunja rekodi ya kuvuka bahari ya Pasifiki akiwa peke yake.
Maafisa wa kikosi cha walinzi wa baharini Marekani kwa sasa wanamtafuta maeneo ya bahari karibu na visiwa vya Hawaii ambapo mashua yake ilionekana ikiwa haina mtu ndani.
Kundi la kumsaidia Bw Guo lilipoteza mawasiliano naye mwendo wa saa 07:00 GMT Jumanne.
Baharia huyo, ambaye alikuwa Mchina wa kwanza kuzunguka dunia kupitia baharini, aliondoka San Francisco mnamo 18 Oktoba akiwa na lengo la kufika Shanghai baada ya siku 20.
Wenzake walipoteza mawasiliano naye na ndege imetumwa kumtafuta eneo la mwisho ambapo alionekana.
Eneo hilo limo karibu kilomita 1,000 kutoka kisiwa cha Oahu, Hawaii.
Rekodi ya sasa ya kuvuka bahari ya Pasifiki kwa mashua mtu akiwa peke yake ni kutumia muda wa siku 21.

No comments:

Post a Comment