Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba
Wadau hao, waliotakiwa kutoa maoni yao tangu wiki iliyopita mbele ya kamati hiyo, waligoma kutoa kwa madai kuwa walipatiwa taarifa za kuwasilisha maoni yao kwenye kamati hiyo katika kipindi kifupi hivyo hawakujiandaa vyema.
Wadau waliohudhuria kikao hicho na kuomba kuongezewa muda ni Jukwaa la Wahariri (TEF), klabu mbalimbali za waandishi wa habari, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), MISATan, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika kikao hicho, wadau hao waliomba kuongezewa muda wa takribani miezi minne ili waweze kushirikisha wadau wengi zaidi kuupitia muswada huo na kutoa maoni yao kwa mrengo mmoja.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, aliongeza siku tisa ili wadau hao wajiandae kutoa maoni yao kwa ajili ya kuboresha muswada huo akibainisha kuwa muda uliotolewa kwa wadau hao tangu awali ulikuwa unatosha.
Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo haitaweza kukamilisha kazi yake ya kupitia na kuboresha muswada huo bila kupata maoni ya wadau ambayo nayo yatasaidia kuuboresha zaidi muswada huo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari na mawasiliano jana, kamati hiyo imepanga kupokea maoni ya wadau hao mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment