Simba iliyoweka kambi yake Morogoro kujiandaa na Ligi Kuu chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake, Mganda Jackson Mayanja waliamua kuwatoa uvivu wachezaji wao kwa kuwakimbiza milimani ili kuwaweka fiti.
Moja ya matatizo ya Simba katika msimu wa hivi karibuni ni wachezaji wake kukosa nguvu jambo lililokuwa likiwapa wakati mgumu wapocheza na timu zinazocheza soka ya nguvu kama Yanga, Prisons, Mwadui, Mbeya City na Azam.
Katika kuhakikisha hali hiyo haijitokezi msimu huu, kocha Omog alisema lengo la mazoezi ya kupanda milima ni kuwaweka fiti na kuwawafanya wachezaji wawe na nguvu na wepesi tayari kucheza na timu yoyote uwanjani.
“Programu ya leo (jana) ni mbio kama tulivyofanya asubuhi na jioni ni mapumziko hadi Jumatatu tutaendelea tena. Lengo ni kuhakikisha wanakuwa na nguvu za kutosha na watakaporudi kuanza msimu wa ligi, wasitikishike na msuli wa mtu yeyote,” alisema Omog.
Katika mazoezi hayo, kocha Omog aligawa makundi mawili kila moja likapewa majukumu yake.
Kundi moja lilizunguka katika vilima vilivyopo eneo la Highlands wakati la pili lenyewe lilikimbia kupitia Chuo cha Ualimu Kigurunyembe hadi Bigwa Mwisho na kurudi. Wachezaji hao walikimbia kwa dakika 45, baada ya hapo wakafanya mazoezi ya viungo kwa ajili ya kukamua mafuta yasiyohitajika mwilini na nyama uzembe kwa dakika 30.
Kujipima kwa Polisi Moro
Baada ya kufanya mazoezi ya nguvu kwa takribani wiki mbili, Simba itaanza kucheza mechi zake za kirafiki Jumanne hii dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Highlands.
“Tutacheza mechi ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Polisi Morogoro baada ya hapo tutaangalia jinsi wachezaji walivyopokea mafunzo na mapungufu yao, nia ni kufanya kazi kwa vitendo,” alisema Omog.
“Kwa sasa kila kitu kinakwenda vizuri, kwa ushirikiano na morali walionao vijana, imani yangu ni kuwa na Simba itakuwa imara tuliyoitarajia,”alisema kocha huyo wa zamani wa Azam FC.
No comments:
Post a Comment