Maelekezo ya Kiongozi wa Chama ( KC ) kwa wanachama wote wa ACT Wazalendo ( KC/01/2016 ).
Tangu
kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 Utawala mpya umekuwa
ukifanya kila juhudi kuminya uwezo wa Vyama vya Siasa kufanya Kazi zake
kwa kisingizio kuwa huu ni wakati wa kufanya Kazi na kwamba Siasa
zisubiri mwaka 2020.
Chama
chetu kilipinga kwa nguvu zote uzuiaji huu wa shughuli za kisiasa kwani
ni kinyume cha Katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa, sheria
namba 5 ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mara kwa Mara.
Mnamo
tarehe 5 Juni 2016 Chama chetu kilifanya Mkutano wa Hadhara Mbagala
jijini Dar Es Salaam na kutangaza Operesheni Linda Demokrasia. Lengo la
Operesheni hiyo ( Tamko la Mbagala 2016 ) ni kuhakikisha kuwa Tanzania
inaendelea kuwa Nchi ya kidemokrasia na kuepuka mwelekeo wa Utawala wa
Imla ambao ni utawala wa kidikteta. Chama chetu asili ya uundwaji wake
ni kupinga tabia za kidikteta tulizokumbana nazo ndani ya Vyama
tulivyokuwamo.
Hivyo
ilibidi tuwe mstari wa mbele kupinga dalili zozote za kuielekeza Nchi
kwenye Uimla. Vyama unaweza kuunda utakapo, Nchi huwezi kuiunda ndio
maana ni LAZIMA Sisi Kama wanachama wa Chama cha Wazalendo kupinga kwa
nguvu zote kuminywa kwa Demokrasia na kuilinda kwa nguvu zetu zote.
Kufuatia
Tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano kwamba shughuli za kisiasa
zimezuiwa kwa niaba yenu nilitaka Vyama vyote vya Siasa nchini na wadau
wengine wa demokrasia kuungana kwa pamoja kukataa Tamko hili ambalo
linavunja Katiba ya Nchi ambayo Rais ameapa kuilinda na kuitetea. Wito
wetu unanukuliwa hapa chini;
"Tunatoa
wito kwa Vyama vyote vya siasa nchini kuunganisha nguvu katika
kuhakikisha tunapigana vita [ dhidi ya udikteta] pamoja. Huu ni wakati
wa vyama vya siasa na wanasiasa kuacha tofauti zao na kupambana kulinda
uhuru wa kufanya siasa wakati wowote kwa mujibu wa Sheria."
Hata
hivyo, hakuna Kiongozi wa Chama chochote kile ambaye aliona umuhimu wa
kuunganisha nguvu na hivyo kujikuta kila Chama kinaendelea na operesheni
zake.
Viongozi
wetu akiwemo Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu walifanya juhudi zote
kuwasiliana na watendaji wenzao wa Vyama vingine ili kufanya Kazi pamoja
japo kwa uratibu lakini hatukupiga hatua yeyote ile.
Hivyo,
Sisi sio sehemu ya operesheni yeyote ile iliyotangazwa na Chama kingine
chochote kile isipokuwa Operesheni Linda Demokrasia ambayo sasa itaitwa
Tamko la Mbagala la Juni 5, 2016.
Akiwa
ziarani mkoani Singida, Rais amefafanua agizo lake la kuzuia mikutano
ya kisiasa. Rais amesema kwamba hajazuia wabunge na madiwani kufanya
mikutano ' KWENYE MAJIMBO YAO'. Kwanza Rais hana mamlaka ya kuruhusu au
kuzuia Kazi za Wabunge na madiwani. Haya ni mamlaka ya KATIBA na sheria
za Nchi. Hivyo ufafanuzi wake hauna maana yeyote ile.
Jambo
la kushtusha ni agizo la Rais kwamba Wabunge hawana mamlaka ya kufanya
mikutano nje ya majimbo yao. Hii ina maana hata Viongozi wa kisiasa
ambao sio wabunge hawataruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa. Hii
HAIKUBALIKI.
Anna
Elisha Mghwira ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, anazuiwaje kufanya
mikutano na wanachama wake nchini? Anazuiwaje kuongeza wanachama?
Lakini mama Anna Mghwira aligombea Urais, kwanini asifanye mikutano
kuwashukuru waliompa Kura japo hazikutosha?
Uchambuzi wa kitaalamu
Ni
dhahiri Serikali ya Awamu ya Tano na sasa Chama tawala wameamua
kubadili mwelekeo wa Nchi kisiasa ( kwa kubana uhuru wa kidemokrasia )
na kiuchumi ( kwa kuelekeza nguvu kwenye uchumi unaoelekezwa/endeshwa na
dola ). Udhibiti wa Vyama vya Siasa ni moja ya hatua ya udhibiti wa
jamii kwa ujumla wake.
Siku
za usoni tutaona udhibiti wa waziwazi wa vyombo vya habari na kwa sasa
tunaona namna Asasi za Kiraia ( CSOs) zilivyo kimya tofauti na miaka
michache ya nyuma. Hizi zimejiweka kimya zenyewe na zitakazoinua sauti
zitafuatiliwa na dola. Yote haya yanaturudisha nyuma katika katika
kujenga Tanzania ya Kidemokrasia na yenye Maendeleo.
Utawala
wowote ' regime ' hutaka kupata nguvu ya wananchi katika kujijengea
uhalali. Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuichukua vita dhidi ya
ufisadi kama njia ya kujijengea uhalali na kwa kweli wananchi wengi
waliochukizwa na vitendo vya kifisadi wanaunga mkono juhudi hizo.
Katika
ziara yake ya Singida, Rais amenza kutumia maneno kama ' mabeberu ' na '
Maadili ya Mwalimu Nyerere ' maneno ambayo hayajawahi kutamkwa na
kinywa chake. Hii inaonyesha kuwa Rais anaanza kukua/kukuzwa kiitikadi
na hii itampa uhalali zaidi mbele ya jamii.
Hata
Uamuzi wake wa kutekeleza maamuzi ya kuhamia Dodoma, na iwapo
atatekeleza, itamjengea zaidi uhalali. Rais atautumia uhalali huu
kujikita katika utawala na kuminya zaidi Demokrasia.
Maelekezo ya Kiongozi wa Chama ( KC )
1.
Chama cha ACT Wazalendo kiliundwa kwa madhumuni ya kurejesha Nchi
kwenye misingi. Kupitia Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha
tumeeleza misingi hiyo kwa kina. Naelekeza kwamba wanachama wote wa ACT
Wazalendo wasome, kuelewa na kujadili Azimio la Tabora na kuchambua
muktadha wake katika mazingira ya sasa ya Siasa za Nchi yetu.
2.
Kila Mwanachama wa ACT Wazalendo asione aibu kuunga mkono maamuzi
yeyote ya Serikali au Chama kingine cha Siasa yanayoendana na Azimio la
Tabora hususan vita dhidi ya ufisadi na kurejeshwa kwa Miiko ya Uongozi.
3.
Kila Mwanachama wa ACT Wazalendo akatae kwa namna anayoweza lakini kwa
Amani mbinu zozote za kuminya Demokrasia nchini. Tamko la Mbagala la
kulinda Demokrasia litumike kuongoza juhudi hizo. Chama chetu
hakijatangaza maandamano na hivyo wanachama wetu wasiingie katika mambo
hayo.
Hata
hivyo kila mwanachama wa Chama chetu aandike barua kwa Rais Magufuli
kwa namna anavyoona yeye kumtaka aache kuingiza Nchi kwenye utawala wa
Imla. Chama chetu kina wanachama 431,120 wenye kadi. Ikulu ikipata barua
200,000 kutoka kila kona ya Nchi itafunguka macho.
Mwisho
Nawataka
wanachama wa Chama Cha ACT Wazalendo kukumbuka kuwa uasili wa Chama
chetu ni kupinga kuburuzwa, ufisadi na Siasa za ujanja ujanja.
Tujitahidi kwa nguvu zetu zote kutofanya yale ambayo Sisi tumeyakataa.
Viongozi wa kuchaguliwa kwenye vyombo vya uwakilishi Kama madiwani na wabunge wawe makini sana kutii Chama na misingi ya chama.
Tuwe
mstari wa mbele kupinga ufisadi kwani rushwa ni adui wa Haki. Tuwe
mstari wa mbele kutaka kurejeshwa kwa Miiko ya Uongozi. Sisi ndio Chama
pekee chenye itikadi iliyo wazi. Tusiammie itikadi yetu popote tulipo na
bila woga wala aibu.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
30/7/2016
something between lines
ReplyDelete