Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga (kushoto) akimkabidhi hundi Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa wakati wa hafla ya makabidhiano madawati ikiwa ni fedha
zilizochangwa na watumishi wa wizara hiyo ikiwa sehemu ya kutekeleza
agizo la Rais Mhe. John Magufuli mapema hii leo katika shule ya Msingi
Chamanzi iliyopo wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam . Picha na
Beatrice Lyimo-MAELEZO
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es salaam
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wamechangia kiasi cha Tsh.
Milioni 100 ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha umma kuhusu zoezi la
upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na Sekondari nchini.
Akikabidhi mchango huo kwa
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa niaba ya watumishi wa wizara hiyo,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Augustine Mahiga amesema kuwa watumishi hao wametoa fedha hizo kwa
shule ya msingi Chamazi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais la
upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari nchini.
Balozi Mahiga amesema Wizara
yake iliwahamasisha watumishi wake walio makao makuu na wale walio
kwenye balozi mbalimbali nje ya nchi kuchangia zoezi hilo la upatikanaji
wa madawati.
“Ili kufanisha upatikanaji wa
fedha hizi Wizara yangu iliwahamasisha watumishi wake wote walio Makao
makuu na wale walio katika balozi zetu duniani kote, wito huu
uliitikiwa kwa ari na hamasa kubwa na kufanikisha kukusanya kiasi cha
Shilingi 100,176,825.52 za kitanzania”alisisitiza Balozi Mahiga
Waziri Mahiga aliongeza kuwa
mara baada ya kukusanya fedha hizo watumishi wa Wizara hiyo waliamua
kumpatia aliyekuwa Mtumishi wa Wizara ambaye sasa ameteuliwa kuwa Mkuu
wa Wilaya ya Manyoni kiasi cha shilingi Milioni 15 kwa ajili ya ununuzi
wa madawati katika Wilaya yake.
Aidha, amesema kiasi fedha
zilizobaki zaidi ya shilingi milioni 85 zilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa
Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa kwa ajili ya mchango wa utengenezaji wa
madawati ya shule ya Msingi Chamazi iliyoko Wilaya ya Temeke Jijini Dar
es Salaam.
Waziri Mahiga aliongeza kuwa
mbali na wizara yake kuwa na majukumu mbalimbali bado inalo jukumu la
kuhakikisha inaitangaza Tanzania ili kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi
wa nchi, na kuongeza kuwa elimu bora ni msingi imara katika kufanikisha
hilo.
No comments:
Post a Comment