Mwananchi alivyobabuka kichwa na miguu.
MARA: Sakata la maji machafu yanayodaiwa yana sumu kutoka mgodi wa dhahabu wa North Mara (Nyamongo) uliopo Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, limeshika kasi baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuamua kuchukua sampuli za maji hayo na kuzipeleka kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara katika nchi za Ujeruman, Ufaransa na Ubelgiji ili ukweli ubainike.
Hatua ya Waziri Muhongo imekuja baada ya kukataa taarifa ya kamati yake iliyotolewa na Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) katika kikao chake na wananchi wilayani hapa.
Kukataa kwake kulitokana na kushinikizwa na wananchi na mbunge wao John Heche wa Jimbo la Tarime Vijijini aliposema kuwa taarifa ya Wizara ya Mazingira na Muungano chini ya ofisi ya makamu wa rais, inasema kuwa maji yana sumu ambayo haikutajwa ni ya aina gani.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza na waathirika wa tukio hilo.
Mama akitoa ushuhuda
Mashaka yake hayo yalitokana na kujitokeza mama na mtoto wake aliyejulikana kwa jina la Ayubu Daniel wa miezi minane akiwa amebabuka ngozi kwa madai kuwa ni kutokana na kuathiriwa na maji ya sumu yanayotiririka kijijini hapo kutoka mgodini.
Hata hivyo, Msemaji wa Mgodi huo, Fatuma Msumi alijitokeza mbele ya kikao hicho na kukiri kuwa mama huyo alifika mgodini hapo mara baada ya mtoto wake kuugua akiomba msaada wa fedha za matibabu ambapo kampuni ilikubali kumsaidia lakini tatizo lake halikusababishwa na maji machafu.
Naye Boazy Range kutoka Kijiji cha Matongo alionesha madhara aliyoyapata kichwani na mikononi, baada ya kuoga maji hayo katika makazi yao.
Kwa utata huo licha ya Prof Muhongo kusema kuwa anachukua sampuli ya maji hayo maeneo yanayotiliwa shaka, alisema kwa usimamizi wa kamati yake hiyo, sampuli zake atapewa Mbunge John Heche naye apeleke kuchunguzwa maabara yoyote ile ili naye apate majibu yake na zoezi kama hilo afanye Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga.
Waziri Muhongo alichukua uamauzi huo baada ya taarifa ya NEMC iliyosomwa na Peres Joshua kutoka makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam kukataliwa na wananchi.
Licha ya wananchi wengi kujitokeza, walidai maji hayo huua mifugo ya wakazi wa Kijiji cha Matongo. Wananchi wa eneo hilo walidai kuwa sampuli ya maji hayo waliipeleka maabara ya Nairobi, Kenya na majibu yakatoka Machi 20, 2015 yaliyobaini kuwa yana sumu na hayafai kwa matumizi ya mifugo na binadamu.
No comments:
Post a Comment