Mkuu
wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akionyesha kitabu cha taarifa
cha mpango mkakati wa kudhibiti virusi vya ukimwi na ugonjwa wa ukimwi
,mpango ambao ni wa miaka mitano ijayo ,baada ya kuzindua mpango huo
jana katika mkutano maalum wa kazi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani
mhandisi Evarist Ndikilo amezindua mpango mkakati wa kudhibiti ukimwi wa
miaka mitano ijayo lengo likiwa kupambana na maambukizi mapya ya gonjwa
hilo.
Amesema mkoa huo ni
miongoni wa mikoa kumi nchini iliyo na kiwango cha maambukizi ya
virusi vya ukimwi juu ambapo una kiwango cha asilimia 5.9 wakati
kitaifa ni 5.1.
Mhandisi Ndikilo
aliyasema hayo ,katika mkutano maalum wa kazi ambao agenda juu ilikuwa
ni kuzindua mpango huo ,uliofanyika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi
ya mkuu wa mkoa wa Pwani,Kibaha.
Alielezea kuwa taarifa
ya matokeo ya tathmini ya maambukizi ya VVU kitaifa iliyofanyika mwaka
2011/2012 mkoa huo ulikadiriwa kuwa na kiwango cha maambukizi ya VVU kwa
kiasi hicho ambacho ni kikubwa.
Mhandisi Ndikilo
alisema kwa kuanza na mpango mkakati huo utasaidia kupunguza kiwango cha
maambukizi ya virusi hivyo mkoani hapo.
“Huu ni mwitiko wa
agizo alilolitoa rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete
alipozindua taarifa ya matokeo ya utafiti wa viashiria vya VVU na ukimwi
na malaria THMIS mwaka 2011/2012”
Mhandisi Ndikilo
alisema Kikwete aliagiza kila mkoa uandae mpango mkakati wa kudhibiti
ugonjwa huo hatari ambao utalenga kudhibiti vichocheo vya maambukizi
kulingana na eneo husika.
Alitaka mkakati ufanyiwe kazi na utekelezaji kwa vitendo pasipo kuuweka kwenye makabati na kuishia kwenye makabrasha.
Aidha mhandisi Ndikilo
aliwaomba viongozi wa dini mkoani humo kushirikiana na serikali
kuhubiri kwa waumini kuwa na maadili mema na kuachana na ngono zembe.
“Mapadre na mashehe
nyie pia ni msaada mkubwa kusaidia hili ,nawaomba tushirikiane kwa
hili licha ya vitabu vya dini kutokubaliana na masuala haya hasa ya
kuhubiri matumizi ya kondom ” alisema mhandisi Ndikilo.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa ushauri wa kutumiwa kwa vikundi vya sanaa na maigizo ili kufikisha ujumbe wa jamii kupitia sanaa.
Alikemea vigodoro na
mikesha isiyo na tija ambayo baadhi ya watu huitumia vibaya na
kusababisha kuugua magonjwa ya zinaa na ukimwi.
Mratibu wa ukimwi mkoani Pwani Grace Tete alieleza kuwa watahakikisha wanatekeleza mpango huo pasipo kuishia kwenye makabati.
Grace alisema mpango
huo utekelezaji wake ni hadi ifikapo 2020 na unalengo la kufikia sifuri
3 ambazo ni maambukizi mapya,ya unyanyapaa na sifuri ya vifo
vitokanavyo na ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Alisema mpango mkakati utatumiwa na halmashauri zote za mkoa kuanzia sasa ili kukabiliana na janga la gonjwa hilo.
Nae msaidizi wa shehe
mkuu na kadhi wa mkoani hapa ,Hamis Mtupa aliwaasa wanandoa waache
michepuko na badala yake wawe waaminifu kwenye ndoa zao ili kujiepusha
na magonjwa ya zinaa.
Mtupa alisema kuhusu
agizo la mkuu wa mkoa wamelipokea hivyo ametoa wito kwa viongozi
wengine wa dini kutenga sehemu ya kutoka elimu juu ya ukimwi.
No comments:
Post a Comment