Sunday, 24 July 2016

Mpango wa elimu bure umedaiwa kuanza kutumiwa vibaya

Mpango wa elimu bure umedaiwa kuanza kutumiwa vibaya baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi mkoani Simiyu kwa kuorodhesha idadi kubwa majina hewa ya wanafunzi  ili shule zao ziweze kupata fedha nyingi huku baadhi ya walimu wa madarasa wakitembea na madaftari ya mahudhurio kwa kuhofia kuongezewa majina hewa.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa wa simiyu  Antony Mtaka amewaagiza wakurugenzi na wakuu wa wilaya kufanya uhakiki wa wanafunzi hewa na watakaobanika kufanya hivyo wawajibishwe.

Agizo hilo amelitoa katika kikao kazi  cha wadau wa  elimu mkoani simiyu kilichokuwa kikijadili  tathimini fupi ya elimu na kutoa dira ya elimu na mikakati madhubuti ya kutatua changamoto zilizopo ambapo ufaulu umepanda kutoka asilimia 40 na kufikia asilimia 60 kitaifa.

Mtaka amesema kuwa wapo baadhi ya wakuu wa shule wasio waaminifu wamekuwa wakiongeza  majina wanafunzi hewa  ili fedha hizo zinazokuja za elimu bure waweze kujinufaisha hivyo lazima uhakiki ufanyike na watakaobainika kuwajibishwa.

Akizungumza mara baada ya majadiliano hayo mkuu wa wilaya ya meatu Dk joseph chilongani ameahidi kutekeleza agizo la kudhibiti utoro mashuleni kwani hakuna kisingizio cha mwanafunzi kukosa mahitaji ya lazima huku akikisitiza kuhakiki wanafunzi hewa.

No comments:

Post a Comment