Saturday, 30 July 2016

Azam FC kumaliza kambi kwa kupimana na Jang'ombe

Timu ya Azam FC itashuka kucheza mechi yake ya kirafiki na timu ya Jang’ombe uwanja wa Amaan ikiwa ni maandalizi ya mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa Agosti 17 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Afisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd Maganga amesema kocha wa timu hiyo Zeben Hernandez atautumia mchezo huo kwa ajili ya kuendelea kuangalia viwango vya wachezaji wa timu hiyo ili kupata kikosi chake cha kwanza.

Jaffar amesema, licha ya kocha huyo kutafuta kikosi cha kwanza katika mchezo huo lakini atautumia mchezo huu pia kutazama uwezo wa wachezaji wa kigeni ambao wanafanya majaribio katika timu hiyo na baada ya hapo wataweka utayari kwa kwa mechi ya Ngao ya Jamii.

Mchezo huo utakuwa wa mwisho kwa Azam FC visiwani humo ambapo kesho inatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuendelea na kambi ya maandalizi ya ngao ya jamii na ligi kuu ya soka Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment