Na: Frank Shija, MAELEZO
Kampuni ya Reli ya Tanzania (TRL)
imefanya mabadiliko ya muda wa Treni ya Abiria kulekea mikoa ya Kigoma
na Mwanza ambapo kuanzia tarehe 02 Agosti 2016 Treni itaanza kuondoka
saa tisa(9) mchana badala ya saa 11 jioni muda wa sasa.
Mabadiliko hayo yametangazwa na
Meneja Uhusiano wa TRL Midladjy Maez wakati akizungumza na waandishi wa
habari Ofisi kwake leo Jijini Dar es Salaam.
Maez amesema kuwa mabadiliko hayo
yamefanyika ili kutoa nafasi kwa treni ya pili ya huduma za Jiji kutoka
kituo Kikuu cha Reli cha Dar es Salaam kwenda Pugu ambayo itaanza kutoa
huduma mapema siku ya Jumatatu ya tarehe 01/08/2016.
Aliongeza kuwa mabadiliko hayo
yanahusu treni za abiria za huduma za kawaida zinazoondoka siku za
Jumanne na Ijuma na kubainisha kuwa kwa upande wa huduma za treni ya
Deluxe zitaendelea na muda wake wa kawaida.
“Uongozi umeamua kufanya
mabadiliko haya kwa sababu za kiusalama zaidi kwani mabadiliko haya
yataepusha muingiliano unaoweza kupelekea ajali na kuongeza kuwa kwa
safari za kutoka Kigoma na Mwanza muda umebaki uleule”. Alisema Maez.
Meneja Uhusiano huyo aliongeza
kuwa huduma za treni ya Jiji kwenda Pugu itakuwa na vituo 10 ambavyoa
alivitaja kuwa ni pamoja na Pugu Stesheni, Gongo la Mboto,FFU Mombasa,
Banana, (njia panda kwenda Stesheni), na karakata.
Vingine ni pamoja na Vingunguti Mbuzi,SS Bhakressa, Kamata na Kituo Kikuu cha reli Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa huduma hiyo
itakuwa na awamu mbili asubuhi na Alasiri ambapo treni ya kwanza
itaondoka kituo cha Pugu saa 12 asubuhi na kuwasili kituo cha Dar es
Salaam sa 12:55 asubuhi na kufanya safari tatu zitakazomalizika saa
05:15 asubuhi. Jioni kutakuwa na safari tatu ambapo treni itaondoka
kituo cha Dar es Salaam saa 09:55 alasiri kwenda Pugu na kuwasili saa
10:50 jioni na safari ya mwisho kutoka Pugu kuja Kituo Kikuu cha Dar es
Salaam saa 03:20 usiku.
No comments:
Post a Comment