



Na Zuena Msuya, Dar Es Salaam
Wizara ya Nishati na Madini
imetoa semina ya siku moja kwa Wakuu wa Mikoa ambayo Bomba la Mafuta
litapita kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini
Tanzania na Makatibu Wakuu wa Wizara zinahusika moja kwa moja na Ujenzi
wa Bomba hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
semina hiyo jijini Dar es salaam, Waziri wa Nishati na Madini Profesa
Sospeter amesema, semina hiyo itawawezesha Viongozi hao kuwa na uwelewa
mpana juu ya ujenzi wa bomba hilo pia kushirikiana kwa karibu na
kufanikisha kukamilisha mradi wa bomba hilo kwa wakati uliopangwa.
Aidha, amesema endapo wahusika
wakuu watafahamu kwa kina mwenendo mzima wa ujenzi bomba la mafuta
kutoka Hoima Uganda hadi bandari ya Tanga hapa nchini, hali hiyo
itasaidia kutoa elimu zaidi kwa wananchi na hivyo kuondoa changamoto
mbalimbali zilizowahi kutokea wakati wa utekelezaji wa miradi mingine
mikubwa iliyotangulia.
Profesa Muhongo ametaja baadhi ya
Wizara ambazo zina husika moja kwa na ujenzi wa bomba hilo kuwa ni
pamoja na Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi,Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi
pamoja na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wizara zingine ni pamoja na
Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Pamoja na Wizara ya Maliasili
na Utalii.
Mradi wa ujenzi wa Bomba la
mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania
utakuwa Mradi wa tatu kwa Ukubwa nchini Tanzania ukitanguliwa na ule wa
Ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Tanzania hadi Zambia(
TAZARA) na Ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mkoa Mtwara hadi Jijini Dar
es salaam.
Bomba hilo litakuwa na urefu wa
kilomita 1,443 na upana wa nchi 12, litagharimu shilingi bilioni 3.5 na
unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment