Na Chrispino Mpinge
Kufuatia majadiliano na vikao
mbalimbali vilivyofanyika mwaka 2005-2010, kumbukumbu zinaonyesha kuwa
suala la uanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) lilifanyiwa kazi kwa ukamilifu
na Serikali za pande zote mbili kwa ushirikiano na Vyama vyote viwili.
Hayo yamesemwa leo na
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (Mb)
wakati akijibu swali la Mhe. Mbunge wa Dimani Hafidh Ali Tahir lenye
kipengele a,b na c lililotaka kujua ni nini matokeo ya Kamati iliyoundwa
na Waziri Mkuu.
Mhe. Nnauye ameeleza
kwamba, kwa kutambua umuhimu wa ZFA kupata uanchama wa FIFA, mwaka 2010
ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba, ukiongozwa na aliyekuwa
Naibu Waziri Kiongozi, Mhe. Juma Shamhuna pamoja na aliyekuwa Naibu
Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Joel Bendera
walikwenda Zurich, Switzerland ambako walikutana na Rais wa FIFA wa
wakati huo.
Aidha, Mhe, Nnauye
amefafanua kuwa, katika msafara huo walifuatana na viongpozi wa TFF na
ZFA na madhumuni ya safari hiyo ilikuwa ni kuwasilisha maombi ya ZFA
kupewa uanachama wa FIFA.
“Mwezi Juni 2011, FIFA
iliiandikia ZFA ikiwajulisha kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo,
isingewezekana Zanzibar kupata Uanachama wa FIFA kwa kuwa wananchama wao
ni nchi zinazotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyoelezwa
katika aya ya 10 ya Katiba yao”, alisema Mhe. Nnauye.
Mhe. Nnauye aliongeza
kuwa, suala la usajili wa TFF au ZFA linafahamika vyema ndani ya
Serikali ya Mapinduzi pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
“Hata hivyo, naomba
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa, uanachama wa TFF katika FIFA upo
kwa mujibu wa muafaka wa pande zote mbili.
Kwa kuzingatia
utaratibu wa FIFA kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo imewaelekeza TFF nao wako tayari kufanya maridhiano na
ZFA ili kukamilisha utaratibu wa wazi wa kukidhi mahitaji ya Zanzibar
kushiriki katika masuala ya FIFA kupitia TFF bila kuathiri ushiriki wa
klabu za Zanzibar katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la
Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).
No comments:
Post a Comment