Na Golden Mwakatobe
Jeshi la Polisi nchini limetoa wito kwa wamiliki wa silahi kujitokeza na kuhakiki silaha zao katika Wilaya wanazoishi kabla ya kumalizika kwa zoezi hilo mnamo Juni 30 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Msemaji wa
Jeshi hilo Kamishna Msaidizi Advera Bulimba alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
“Serikali imetoa muda wa miezi
mitatu kukamilisha zoezi hili muhimu na tayari miezi miwili imepita
hivyo wale ambao bado hawajahakiki silaha zao kuzikakiki sasa kabla ya
Juni 30 ili kuepukana na usumbufu” alisema Kamshna Msaidizi Bulimba na
kuongeza kuwa:
“Natoa wito kwa watu wote
wanaomiliki silaha kinyume na sheria kusalimisha silaha hizo katika
vituo vya polisi, ofisi za serikali na kwenye nyumba za ibada na
watakaofanya hivyo ndani ya muda ulipangwa hawatachukuliwa hatua zozote
za kisheria”.
Aliongeza kuwa baada ya muda
ulipangwa na Serikali kupita na wamiliki hawajahakiki silaha zao Jeshi
la Polisi nchini litaendesha operesheni kali kuwakamata wale ambao
hawakujitokeza katika zoezi la uhakiki na hatua kali zitachukuliwa
ikiwemo kufutiwa leseni na silaha zao kutaifishwa na kuwa mali ya
Serikali.
Aliwaomba ndugu wa wale walikuwa
wakimiliki silaha ambao wamefariki au ni wagonjwa wasalimishe silaha
hizo katika vituo vya Polisi kwa niaba ya ndugu zao ndani ya kipindi cha
uhakiki wa silaha.
Zoezi la uhakiki wa silaha
lilianza Machi 21 mwaka huu kufuatana na sheria ya usimamizi wa silaha
na risasi ya mwaka 2015, ambapo kifungu cha 66 cha sheria hiyo kinamtaka
kila mmiliki kuhakiki kumbukumbu za silaha yake au risasi pale
anapoamriwa na mamlaka.
Lengo la kuhakiki kumbukumbu za
wamiliki wa silaha ni kupata taarifa sahihi za wamiliki hao
zitakazosaidia kubaini wale wote wanaomiliki kinyume na sheria,
kuwafahamu wamiliki waliohama na kuhamia makazi mapya, kuwafahamu
wamiliki waliofariki ili kuzuia vitendo vya uhalifu na uvunjwaji wa
amani nchini.
No comments:
Post a Comment