Na Lydia Churi – Geita
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amezitaka Mahakama za mkoa wa Geita
kuhakikisha zinamaliza kesi kwa wakati ili kutekeleza lengo lililowekwa
na Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza na watumishi wa
Mahakama jana mkoani Geita, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania
ilijiwekea malengo ya kumaliza kesi katika mahakama zake kwa wakati
kulingana na aina ya mahakama.
Alisema kwa mahakama za Hakimu
Mkazi, mahakama za Wilaya pamoja na Mahakama za Mwanzo lengo lilikuwa
ni kumaliza kesi zote ndani ya mwaka mmoja ili kuwafanya wananchi
kuendelea kuwa na imani na mahakama zao kwa kuwa ni zaidi ya asilimia 90
ya wananchi wanahudumiwa na mahakama hizo.
Jaji Mkuu alisema kwa mahakama za
Mwanzo ambazo ziko 970 nchini kote lengo lilikuwa ni kuhakikisha
hazikai na kesi kwa zaidi ya miezi sita kwa kuwa ndizo mahakama
zinazohudumia wananchi wengi zaidi.
Alisema ili kuziwezesha Mahakama
kutekeleza lengo walilojiwekea, tayari Mahakama ya Tanzania imeajiri
Mahakimu wapya 107 ambao watasambazwa kwenye Mahakama zote za Mwanzo
nchini kwa ajili yakwendakutoa huduma ya msingi ya mahakama ya kutenda
haki kwa wananchi wa Tanzania.
Akizungumzia suala la utoaji wa
nakala za hukumu, Jaji Mkuu amezitaka Mahakama za mkoa wa Geita kutoa
nakala hizo mapema iwezekanavyo ili kutoa haki ya kukata rufaa kwa
wananchi ambao hawakuridhishwa na hukumu walizopewa katika kesi zao.
Alisema Mahakama ya Tanzania
itaongeza idadi ya Makatibu Mahususi na kuongeza vifaa katika Mahakama
zake ili kuongeza kasi ya uchapaji wa nakala za hukumu. Alisema asilimia
80 ya bajeti inayotolewa kwa muhimili huo imetengwa kwa ajili ya
kuendesha kesi katika mahakama za Mwanzo, Wilaya na zile za Hakimu
Mkazi.
Jaji Mkuu anaendelea na zaira
yake katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ambapo anatembelea mikoa
Mwanza, Geita na Mara ili kukagua shughuli za kimahakama katika kanda
hiyo
No comments:
Post a Comment