Na Kalonga Kasati
Serikali imewataka wauzaji wa
vifaa vya Mawasiliano vya mkononi (mobile devices) kuacha mara moja
tabia ya kubadilisha namba tambulishi (‘kuflash’) za vifaa hivyo kwani
watakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka 10 au faini isiyopungua
milioni 30 au vyote viwili.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja
Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent
Mungy wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam.
“Namba tambulishi (IMEI) za vifaa
vyote vya Mawasiliano ya mkononi ambavyo vimeibiwa,vimeharibika,kupotea
au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano
havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo
tarehe 16 June 2016. “Aalisema Mungy.
Akizungumazia kampeni ya
kuelimisha umma kuhusu matumizi ya simu zote zisizokidhi viwango, Mungy
alibainisha kuwa idadi ya simu hizo imeshuka kutokana na elimu ambayo
wameitoa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema lengo la elimu hiyo kwa
umma ni kujenga uwezo kwa wananchi kutambua simu zisizokidhi vigezo
kabla ya kufika ukomo wa matumizi ya simu bandia nchini.
Mungy alifafanua kuwa uchambuzi wa
IMEI unaonyesha kuwa hadi Februari,2016 idadi ya namba tambulishi
ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia 3 ambapo namba
tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 18 na simu
halisi zilikuwa sawa na asilimia 79.
“Kwa mwezi Machi 2016 ulionyesha
kuwa Idadi ya namba tambulishi ambazo hazina viwango ni asilimia 4, na
idadi ya zile zilizonakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 13 ambapo
uchambuzi huu umehusisha taarifa za kampuni zote za simu nchini’’.
Alifafanua Mungy.
Aliongeza kuwa matokeo hayo mazuri
ni matunda ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Mamlaka hiyo, Shirika la
viwango Tanzania (TBS),Tume ya ushindani (FCC),kampuni za simu, pamoja
na wadau wengine katika kuelimisha umma juu ya uhakiki wa simu walizo
azo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu
ikiwemo kuzihakiki ubora wake.
Kwa Upande Wake Kaimu Naibu
Mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Mawasiliano wa Mamlaka hiyo
Injinia Gabriel Mruma amesema kuwa ni vyema watanzania wakajenga
utamaduni wa kununua simu zenye ubora kuepuka usumbufu wakati Tanzania
inapoelekea ukomo wa matumizi ya simu bandia.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni
Taasisi ya Serikali yenye Dhamana ya kusimamia shughuli za Mawasiliano
ya Kielektroniki na Posta hapa nchini.
Kuwepo kwa Sheria ya Mawasiliano
ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na Kanuni zake za mwaka
2011 kumewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa rajisi ya namba za Utambulisho
wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
No comments:
Post a Comment