Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza
na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na wadau wa Sekta ya
Mawasiliano (hawapo pichani), wakati uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni
hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es Salaam
Mjumbe
wa Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bi. Edwina Lupembe
akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa, katika hafla ya uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni hiyo
na huduma ya 4G LTE
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha
Kazaura akielezea mafanikio ya TTCL kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika hafla ya
uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es
Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizindua
nembo mpya ya Kampuni ya Simu ya Tanzania (TTCL), jijini Dar es Salam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akijadiliana
jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dkt.
Kamugisha Kazaura, wakati wa halfla ya uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni
hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), wakifatilia sherehe
za uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar
es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Kampuni ya
Simu ya (TTCL), kuwa wabunifu ili kuhimili ushindani wa soko katika
sekta ya mawasiliano na hivyo kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida.
Akizungumza wakati akizindua
nembo mpya ya kampuni ya TTCL na huduma ya 4G LTE inayowezesha huduma ya
mawasiliano ya sauti na data kwa haraka Prof. Mbarawa amesema huu ni
wakati wa kubadili mtazamo na kufanya kazi kisasa ili kuvutia wananchi
kutumia huduma za TTCL.
“TTCL lazima mubadilike ili
muweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia na hivyo
kumudu ushindani uliopo sasa katika sekta ya mawasiliano”, amesema
Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka TTCL kuhakikisha kituo mahiri cha kutunzia taarifa (Data Centre), kinaanza mapema mwezi Juni ili kuwezesha wadau wengi kunufaika na kituo hicho.
Prof. Mbarawa amesema Serikali
inaunga mkono TTCL na imetenga masafa ya 800 MHZ ambayo yataiwezesha
TTCL kushindana na makampuni mengine ya watoa huduma ya mawasiliano na
kuwaunganisha wateja wengi kutumia huduma za mawasiliano na data.
“Uzinduzi wa nembo mpya ya TTCL
na huduma ya masafa ya 4G LTE uendane na ubunifu kwa wafanyakazi ili
muwavutie watumiaji wengi wa simu na hivyo kupata soko kubwa na kuifanya
TTCL kuchangia kikamilifu pato la taifa”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema mawasiliano
ni kiungo muhimu cha kufanikisha ukuaji wa sekta za kilimo, taasisi za
fedha, uwekezaji, ujasiliamali na utendaji kazi wa Serikali na sekta
binafsi hivyo ubunifu katika utendaji utaiwezesha TTCL mpya kufikia
malengo yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amewataka wananchi kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhusu namna ya kuzitambua simu na vifaa
feki na hatua za kufuata ili ifikapo Juni 16 zoezi la kuzifunga simu
feki litakapotekelezwa wasiathirike.
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bi. Edwina Lupembe amesisitiza kwamba TTCL
imejipanga kuboresha huduma za fedha ili kuwezesha watumiaji wengi wa
kampuni hiyo kunufaika na huduma ya kutuma na kupokea fedha.
“Tumekamilisha mradi mkubwa wa
kusimika mitambo ya GSM, UMTS na LTE ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa
huduma ya mawasiliano 2G, 3G na 4G”, amesema Bi. Lupembe
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL
Dkt. Kamugisha Kazaura amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa mabadiliko ya
muonekano wa TTCL yataendana na mtazamo mpya wa wafanyakazi wenye lengo
la kuiwezesha kampuni hiyo kuwa ya kisasa hapa nchini.
Amesema TTCL imejipanga kuboresha
simu za mezani, mkononi, na huduma za intaneti ya haraka ili iweze
kupata wateja wengi na hivyo kuongeza mapato yake.
“Teknolojia ya 2G GSM, 3G UMTS na
LTE imeongeza nguvu kwa kampuni yetu kuleta ushindani katika soko la
mawasiliano na zitaendelea kuongeza ufanisi na ubunifu wa huduma zetu
kwa bei nafuu”, amesisitiza Dkt. Kazaura.
Tayari huduma ya 4G LTE inapatikana katika maeneo mengi ya Ilala, Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment