Friday, 27 May 2016

RC aitaka NHIF kuwa wabunifu ili kuongeza wanachama


index 
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Saidi Meck Sadik ametoa rai kwa watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kubuni mbinu mpya za kuwahudumia wanachama wao ili kuhamasisha watanzania wengi kujiunga na mfuko huo.


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya wa Siha Dkt. Charles Mlingwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa mfuko huo uliofanyika Mkoani humo.

Mhe. Meck Sadik amesema kuwa Baraza la wafanyakazi ndiyo chombo sahihi cha uwakilishi wa sauti za watumishi katika kupanga malengo ya Taasisi pia ni chombo cha kutatua migogoro ya kikazi na hivyo kumaliza mapema tofauti zinazojitokeza katika sehemu za kazi kabla hazijaathiri utendaji. 

“Kutokana na umuhimu wa huduma zenu kwa umma, Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wenu linatakiwa lichukue sura mpya na kuwa ni mahali pa ubunifu na kisima cha kuibua mbinu mpya za kuwahudumia vizuri wanachama wenu na kujua namna gani mtaendelea kuwavutia Watanzania wengi zaidi kujiunga na Mfuko”,alisema Meck Sadik. 

Mhe. Meck Sadik ameongeza kuwa anawapongeza kwa ubunifu wao wa kubuni mipango mbalimbali ya uchangiaji inayolenga kuwafikia watanzania wa makundi mbalimbali kulingana na hali zao za vipato na uwezo wao wa kuchangia.

“Hali halisi ya uchumi wa watanzania mnaifahamu, siyo watu wengi wenye uwezo wa kugharamia matibabu kwa fedha taslimu hivyo, huduma za matibabu kupitia Mfuko huu ni ukombozi mkubwa kwa kundi kubwa la watanzania”, alisema Meck Sadik.

Aidha, Mhe. Meck Sadik amewakumbusha  wajumbe wa Baraza hilo kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya wafanyakazi na uongozi wa Mfuko kwa hiyo, wana wajibu wa kuyaelewa malengo ya Taisisi yao kiutendaji na kuyawasilisha kwa wafanyazi wenzao wakiwa kama wamiliki wa kile walichokubaliana na uongozi kuwa ndiyo dira na mwelekeo wa taasisi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernald Konga amesema kuwa mfuko huo utaendelea kushirikiana na Serikali, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa dawa nchini.

“Tunajua kuwa upungufu wa dawa katika vituo vya matibabu umekuwa ni mojawapo ya kero kubwa katika sekta ya afya. Ili kuondokana na kero hiyo, Mfuko umeanza kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na upungufu huo kwa kuanzisha mpango maalumu wa kutoa mikopo ya dawa kwa watoa huduma waliosajiliwa ili kuhakikisha kuwa wanachama wetu na watanzania kwa ujumla wanapata dawa kila wanapokwenda kupata huduma za matibabu”,alisema Konga.
Chimbuko la Mabaraza ya Wafanyakazi linatokana na Agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 lililoagiza kuwa mahali popote penye wafanyakazi wa kudumu kumi na kuendelea panatakiwa pawe na chombo cha kuwawakilisha.

No comments:

Post a Comment