Meneja wa Afya na Usalama kazini wa TANESCO, Mhandisi Majige Mabulla.
Na Golden Mwakatobe
Shirika la Umeme Tanzania Nchini
(TANESCO) limewataka wateja wake kuhakikisha wanaunganishiwa umeme na
mafundi au wakandarasi waliosajiliwa na shirika hilo ili kupunguza ajali
za moto.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Meneja wa Afya na Usalama kazini wa TANESCO, Mhandisi Majige
Mabulla alipokua akiongea na waandishi wa habari juu ya vyanzo vya ajali
za moto vinavyosababishwa na umeme.
Mhandisi Mabulla alisema kuwa
matukio ya moto yanayosababishwa na umeme hutokea kutokana na kuzalishwa
kwa joto kali ndani ya nyaya kunakosababishwa na umeme kuwa mkubwa
kuliko uwezo, kulegea kwa maungio ya nyaya pamoja na radi au nyaya za
umeme kuangukia juu ya paa la nyumba.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mabulla
aliongeza kuwa ajali za moto zinazosababishwa na umeme huanza kama
unavyoanza moto wa kiberiti au viwashio vinginevyo vya moto na husambaa
haraka kwa kutegemea na aina ya vitu vilivyopo kwenye eneo husika kwa
kuwa baadhi ya vitu hushika moto haraka na kuenea kwa kasi.
“Ajali za moto zinazosababishwa
na umeme ni ngumu kutokea kama umeme utasukwa na mtaalam aliyebobea
kwenye fani hiyo, TANESCO tunatoa wito kwa wateja wetu kuhakikisha
wanafungiwa umeme na fundi au mkandarasi aliyesajiliwa na kampuni
yetu,”alisema Mabulla.
Pia Mhandisi Mabulla alisema ili
kuepukana na ajali za moto zinazotokana na hitilafu za umeme wateja
wanapaswa ;kuepuka kupitisha nyaya za umeme juu ya paa za nyumba,
kutokuunganisha umeme kutoka nyumba moja kwenda nyingine bila kupata
maelekeza kutoka TANESCO.
Aidha Mhandisi Mabula alisema
wateja pia wanapaswa kuhakikisha mfumo wa umeme unapitiwa upya kila
baada ya miaka mitano pamoja na kuwa makini katika utumiaji wa vifaa
vinavyotumia umeme kama vile pasi, hita za umeme.
No comments:
Post a Comment