WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa mambo ya malikale na
uhifadhi wa urithi asilia (natural heritage) watafute mbinu
zitakazoimarisha utunzaji wa rasilmali hizo bila kuathiri mifumo ya
uchumi ya nchi zinazoendelea.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Mei
31, 2016), wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa siku nne unaojadili
Uhifadhi wa Urithi wa Dunia wa Afrika kama Nyenzo ya kuleta Maendeleo
Endelevu ulioanza leo kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha
(AICC) jijini Arusha.
Waziri Mkuu amesema kuna baadhi
ya nchi ambazo ni maskini sana lakini zimebarikiwa kuwa na rasilmali
kama madini na gesi asilia lakini kwa sababu rasilmali hizo ziko karibu
sana na vivutio vya urithi asilia wa dunia, watu wa nchi hizo wanazuiwa
kuchuma rasilmali zao ili wasiharibu vivutio hivyo.
“Tunatambua umuhimu wa kutunza
rasilmali na vivutio vya urithi asilia. Hivi ni kwa nini zisitafutwe
teknolojia zinazofaa ambazo zitaruhusu uvunaji wa gesi asilia na madini
bila kuathiri uhifadhi wa vivutio vya urithi asilia wa dunia (world
heritage sites)?”, alihoji Waziri Mkuu.
“Serikali za nchi za Kiafrika
zinahitaji suluhisho kama hili wakati zikiendelea kutafuta njia sahihi
za kuwianisha uhifadhi wa vivutio vya urithi wa dunia na changamoto ya
kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” amesema.
“Sisi viongozi ambao wengi wetu
ni wanasiasa, hatukatai ushauri wa wataalamu lakini tunawasihi baadhi
yenu ambao mnashiriki mkutano huu muhimu, mtafute njia mbadala za
kufumbua tatizo hili badala ya kuendelea kutegemea njia za kizamani za
kukabiliana na changamoto kama hizi ili sote tuweze kunufaika na
rasilmali zilizopo ikiwa ni pamoja na kutunza vivutio vya urithi asilia
wa dunia,” aliongeza.
Amesema kama rasilmali hizo
zitachambuliwa vizuri na kwa njia sahihi bila kuathiri vivutio vya
urithi wa dunia, ni dhahiri kuwa zitaingiza mapato ambayo kiuchumi
yatasaidia kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi ambao pia watasaidia
kwenye uhifadhi wa vivutio hivyo.
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Tanzania
imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi zikiwemo za ardhini (madini),
misitu, wanyama na maeneo ya kihistoria na kusisitiza kuwa Watanzania
wana jukumu la kuzilinda ili zilete tija kwa wananchi wote.
“Tukizitunza rasilmali zetu
zitasaidia kupata mapato kutokana na utalii Serikali itapeleka sehemu ya
mapato haya katika miradi mbalimbali na hivyo kuchangia kwenye pato la
Taifa,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema Tanzania itaendelea
kushirikiana na UNESCO hasa katika masuala yanayohusu uhifadhi wa
vivutio vya dunia kutokana na umuhimu wake kwenye maendeleo endelevu.
Alisema wizara yake imelenga
kusimamia, kuendeleza na kuimarisha utunzaji wa maliasili na uhifadhi wa
vivutio asilia na vya kiutamaduni (natural and cultural heritage) kwa
kushirikiana na wadau wengine hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Uhifadhi
Malikale wa UNESCO, Dk. Mechtild Rossler aliwataka washiriki wa mkutano
huo kutoka nchi mbalimbali duniani wawe tayari kupitia upya shughuli
zinazotekelezwa katika eneo la urithi wa dunia na kuangalia wajibu wa
nchi za Kiafrika katika kuandaa mwelekeo wa miaka ijayo.
Alisema katika miaka 40 ya
utendaji wa UNESCO, idadi ya vivutio vya urithi wa dunia imeongezeka na
kufikia 89 ambapo kati ya hivyo viko baadhi vinakavyobiliwa na
changamoto ya kufutika kutokana na athari za kigaidi, matukio ya kivita
na kazi za kibinadamu.
“Vivutio 16 kati ya 48 viko
katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na hivi
vinakabiliwa na tishio la kupotea kutokana na vita, harakati za kigaidi
na shughuli za kiuchumi za kibinadamu zikiwemo uchimbaji wa madini na
gesi asilia,” alisema.
Aliwataka washiriki wa mkutano
huo wakumbuke kuwa vivutio vya urithi wa dunia ni vielelezo vya jamii na
pia huchangia uchumi kwa kutoa ajira kwenye jamii husika.
Mkutano huo unaohudhuriwa na
washiriki zaidi ya 150 kutoka nchi mbalimbali duniani, unajumuisha
washiriki kutoka nchi 36 zikiwemo nchi 12 ambazo ni za nje ya bara la
Afrika.
Waziri Mkuu amerejea mjini Dodoma mchana huu kuendelea na vikao vya Bunge
No comments:
Post a Comment