Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye makazi yake jijini Dar es salaam.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali itaagiza kutoka nje ya nchi tani 70,000 za sukari
ambapo kati ya hizo, tani 11,957 zimeshawasili nchini na zitaanza
kusambazwa kesho (Jumatano).
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumanne, Mei 10, 2016) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye
mkutano uliofanyika nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akitoa ufafanuzi wa sukari ambayo
imekwishawasili nchini, Waziri Mkuu alisema tani 2,000 zitapelekwa mikoa
ya Kaskazini, tani 3,000 (mikoa ya Kanda ya Ziwa), tani 2,000 (mikoa ya
Kusini), tani 2,000 (Nyanda za Juu Kusini) na tani 2,000 (mikoa ya
Kanda ya Kati).
“Tani nyingine 24,000 za sukari
zitawasili Ijumaa hii na hadi zitoke bandarini itakuwa kama Jumapili kwa
hiyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu. Tani nyingine 20,000
zitawasili baadaye, ama mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi Juni,”
alisema Waziri Mkuu.
Amesema anawataka Watanzania
wasihofu kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani
umesababishwa na watu wachache. “Mheshimiwa Rais ameagiza watu
waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe. Lakini pia
tunaagiza kwa muda mfupi kwa sababu viwanda vyetu vinatarajia kuanza
uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.
Amewataka wasambazaji wa sukari
waziuze kwa wafanyabishara wadogo ili wao wawawuzie wananchi kwa bei
elekezi ya sh. 1,800. Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
kuhakikisha wanasimamia zoezi la ukaguzi ili kubaini zaidi wale
waliohodhi bidhaa hiyo.
Akifafanua kuhusu mkakati wa
Serikali kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, Waziri Mkuu amesema nia
ya Serikali ni kuhakikisha tatizo la uhaba wa sukari nchini linakwisha
ifikapo 2019. “Wananchi wasiogope, Serikali imechukua hatua kwa udhibiti
mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani,” alisema.
“Tunao mkakati wa kuboresha
viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa ubia na wawekezaji
kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo matatu tuliyotenga
kwa ajili hiyo,” alisema.
“Serikali imetenga maeneo matatu
yanayofaa kwa kilimo cha miwa huko Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma. Huko
wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa
unapanda mwaka kwa mwaka hadi tutakapoweza kuimaliza hii gap iliyopo,”
alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 10, 2016.
No comments:
Post a Comment