Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka
Watendaji wakuu, Mameneja na Wazalishaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme
nchini (TEMESA), kutumia maarifa na taaluma zao ili kuboresha utendaji
kazi wa wakala huo na kuongeza mapato.
Akizungumza wakati
akifungua kikao kazi cha TEMESA Taifa mkoani Morogoro, Prof. Mbarawa
amewataka watendaji wa temesa kubadili mfumo wa utendaji na kufanya kazi
kwa kuzingatia matokeo na faida.
“Tengenezeni magari 60 kwa siku muone namna mtakavyopata wateja wengi na kuongeza mapato”, amesema Prof. Mbarawa.
Kikao kazi hicho chenye
malengo ya kuboreshaj utendaji wa wakala huo kitajadili kwa kina
changamoto mbalimbali zinazoikabili TEMESA na kutengeneza mpango wa
kuboresha huduma zao.
“Tumieni elimu
mliyonayo kwa ajili ya maslahi ya watanzania na kuibadilisha TEMESA hii
kuwa ya tofauti na ya pekee”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa
amehimiza Wakala huo kuhakikisha wanadhibiti mapato na matumizi ya mfumo
wa kielektroniki kwenye vivuko vyote ili kukuza na kujiendesha kwa
vivuko vyenyewe.
Amesema mpaka sasa TEMESA ina jumla ya vivuko 27 lakini mapato yake bado yapo chini ya inavyotegemewa
na kushindwa kumudu hata matengenezo ya wakati ya vivuko hivyo.
Wakala huo pia
umesisitizwa juu ya usimamizi wa kina wa usalama wa vivuko na kanuni za
usafiri wa majini ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe wa kutofuata
kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Andaeni kozi fupi kwa
ajili ya watumishi wanaosimamia vivuko na kuja na mikakati madhubuti ya
jinsi ya kuziepuka ajali ambazo zinaweza kuepukika”, amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Prof. MBARAWA amewataka
TEMESA kutengeneza magari yote ya serikali na kutafuta soko katika
magari ya watu binafsi ili kuongeza mapato na ufanisi kwa wakala huo.
“Bado mmelala,
hamjaamka, nataka temesa itengeneze magari yote ya serikali hadi
kufikia asilimia 65 ya matengenezo, tumieni fursa hii ya wizara yenye
taasisi nyingi ili kufanya biashara na kujilipa wenyewe na kwani
inajitosheleza kukua”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Ameongeza kuwa temesa
wamepewa rasiliamali zote hivyo ni lazima wafanye kazi na kujisimamia
wenyewe kwa kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza mahitaji ya watanzania.
Kwa upande wake Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Eng.
Manase Ole
Kujan amemhakikishia Waziri kuandaa mikakati madhubuti ya kuikuza wakala
huo kwa kutoa huduma bora zinazolingana na thamani ya fedha yenyewe kwa
wateja wake.
Katika Hatua nyingine
Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa daraja la Ruvu chini katika
barabara ya Msata-Bagamoyo lenye urefu wa mita 140 na kumtaka Mkandarasi
Estim Construction kuhakikisha daraja hilo linakamilika ifikapo Oktoba
mwaka huu.
Aidha amemuagiza Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Pwani Eng. Tumainieli
Sarakikya kuhakikisha kipande cha barabara kilichobakia katika barabara
ya Msata-Bagamoyo kinaunganishwa ifikapo Februari mwakani.
“Hakikisheni wananchi
hawavamii maeneo ya hifadhi ya barabara kwani kufanya hivyo ni kosa
kisheria na tutachukua hatua kali kwa watakaovunja sheria ya barabara”,
amesisitiza Waziri Mbarawa.
Zaidi ya Shilingi Bilioni 127 zimetumika katika ujenzi wa barabara ya Msata-Bagamoyo yenye urefu wa km 63.
No comments:
Post a Comment