Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika – ADB kwenye Kituo cha Mikutano cha Mlungushi kilichopo Lusaka
Zambia , Mei 24, 2016. Wengine pichani kutoka kushoto ni Makamu wa Rais
wa Nigeria, Prof. Yemi Osinbojo, Rais wa Chad, Idriss Debyo, Rais wa
Zambia, Edgar Lungu na Waziri Mkuu wa Msumbiji, Carlos Agostino do
Rosario (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hadi sasa Serikali imekwishapokea maombi 52 kutoka makampuni
mbalimbali ambayo yanataka kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini
Tanzania.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
jana jioni (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati akizungumza na Watanzania
waishio Zambia katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania
jijini Lusaka, Zambia.
“Haya maombi yamekwishapokelewa
na wenye makampuni wamekwishahojiwa kuangalia uwezo walionao katika
suala zima la uwekezaji wanaotaka kuufanya, na tukiwapata wenye uwezo na
wenye nia ya dhati watapatiwa miradi ya kuiendesha,” alisema.
Aliwataka Watanzania hao waishio
Zambia watumie fursa ya uwepo wao huko kutafuta marafiki ambao wanaweza
kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali nchini kwani Serikali peke yake
haiwezi kufanya kila kitu wakati wananchi wanahitaji kupatiwa huduma
muhimu.
“Serikali peke yake haiwezi
kufanya kazi ya uwekezaji kwa hiyo tunahitaji kushirikiana na sekta
binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo na ndiyo maana
kule kwenye mkutano nimewaeleza washiriki kwamba milango ya uwekezaji
Tanzania iko wazi.
Alisema kupatikana kwa umeme wa
uhakika kutawezesha wananchi wengi zaidi kujiingiza katika shughuli za
kiuchumi na hivyo kuinua uchumi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa
ujumla.
Alisema malengo ya Serikali ya
awamu ya tano ni kuona kuwa nchi inakuwa na mitambo mingi ya kuzalisha
umeme na umeme wote unaozalishwa na mitambo hiyo inaunganishwa na gridi
ya Taifa ili kuondokana na tatizo la mgao wa umeme nchini.
Alisema Tanzania ina vyanzo vingi
vya nishati vikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji,
upepo, nishati ya joto kutoka ardhini (geothermal energy) na nishati
inayotokana na vinyesi vya mifugo (biomass) ambayo alisema vinatumika
kwa watu wachache (siyo kitaifa).
Alisema kupatikana kwa gesi
asilia nchini kumeleta neema ambapo mabomba ya gesi yamekwishajengwa
kutoka Mtwara hadi Kinyerezi na kutoka Kilwa-Songosongo hadi Dar es
Salaam. “Sasa hivi kuna utafiti unaendelea juu ya uwezekano wa kusambaza
gesi ya kupikia majumbani. Tumeanza pale Mikocheni (DSM) na sasa hivi
wanafanya utafiti mwingine kule Mtwara ili wananchi waweze kutumia gesi
hii kupikia badala ya mkaa,” alisema.
Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye
makaa ya mawe, Waziri Mkuu alisema Serikali imelenga kutumia makaa ya
mawe ili kuendeshea mitambo ya kwenye viwanda vikubwa badala ya kutumia
umeme au mafuta ya dizeli kama inavyofanyika sasa. “Baadhi ya wenye
viwanda wanabadilisha mifumo ya kuendeshea mashine zao ili iweze
kuendana na teknolojia ya makaa ya mawe pindi tu uchimbaji ukishika
kasi,” alisema.
Akifafanua kuhusu juhudi za
Serikali katika kusambaza nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema tangu
kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji zaidi ya 3,000
katika ya vijiji 12,000 vilivyopo nchini vimefikiwa na nishati ya umeme.
“Tulianza na REA awamu ya kwanza,
awamu ya pili na sasa tunaenda awamu ya tatu. Hata mkipiga simu kwa
ndugu zenu vijijini, mtakuta katika kila kata kuna vijiji kati ya vinne
hadi vitano ambavyo vimefikiwa na nishati ya umeme kupitia mradi wa
REA,” alisema.
Waziri Mkuu amerejea nchini leo (Jumatano, Mei 25, 2016).
No comments:
Post a Comment