WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vita inayoendeshwa na Serikali ya
awamu ya tano dhidi ya wala rushwa na wale wanaofanya ufisadi siyo nguvu
ya soda kama wengi wanavyofikiri.
“Serikali ya awamu ya
tano imedhamiria kupambana na wala rushwa na mafisadi. Wala hatutanii.
Hawa tutacheza nao na wala wasidhani vita hii ni nguvu ya soda.
Tutaendelea kuwasaka hadi tufike mwisho,” alisema Waziri Mkuu wakati
akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika
kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia juzi jioni (Jumanne,
Mei 24, 2016).
“Hatutaki tabia
iliyokuwepo ya mwananchi anakuja ofisini kutaka huduma lakini
hasikilizwi hadi atoe chochote, sisi hiyo tabia hatutaki kuisikia
kabisa. Tumedhamiria kurudisha heshima kwenye utumishi wa umma na
nimeanza kupata faraja kwani sasa hivi (nimeambiwa) katika baadhi ya
taasisi unasikia mtu akiulizwa una shida gani, nenda pale, jambo ambalo
zamani halikuwepo,” alisema.
Alisema Serikali
imeamua kupigia debe dhana ya utumishi wenye uadilifu kwa sababu huo ni
utamaduni mpya. “Ni kipindi kigumu kidogo cha mabadiliko lakini
tumesimamia mabadiliko haya na ndiyo maana watumishi wote
tumewasisitizia kuwa suala la uaminifu, uadilifu na uwajibikaji ni
muhimu,” alisema na kuongeza:
“Hatutamvumilia
mtumishi yeyote ambaye hatakuwa tayari kuwatumikia Watanzania au
atakayeendekeza uzembe lakini pia hatutamuonea mtu yeyote. Hapa
tunasisitiza usawa na hatutaki kutengeneza gap kati ya mwananchi
mtumishi na wa mwananchi wa kawaida, tunataka kila mwananchi aione
Tanzania ni nchi yake na kila kinachozalishwa ni sehemu yake. Tukifika
hapo, tunaamini kila mmoja ataweza kuisemea nchi yake.”
Akizungumzia kuhusu
ubadhirifu wa fedha za umma, Waziri Mkuu alionya kwamba Serikali imelipa
kipaumbele suala la uaminifu na uadilifu kwenye fedha za Serikali na
kwamba haitakuwa tayari kuona fedha hizo zikifujwa.
“Hivi sasa Serikali
imetenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha hizo
zitaenda vijijini. Tunataka zikafanye kazi iliyokusudiwa, na wale
wadokozi wajue kuwa wamekalia kaa la moto,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema watumishi wa
umma wana wajibu wa kusimamia kazi zilizopangwa na kuhakikisha miradi
iliyolengwa inakamilika. “Kama fedha zimeletwa kujenga zahanati simamia
zahanati ijengwe na ni lazima zahanati hiyo ionekane,” alisema.
Alisema bajeti ya mwaka
huu imeongezeka kutoka sh. trilioni 21 hadi trilioni 29 lengo kuu
likiwa ni kuleta maendeleo kwa wananchi. “Ndiyo maana tumepandisha
bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 27 hadi asilimia 40. Ole wake
atakayepokea fedha hizi halafu zisifanye kazi yake, ukiipoteza wewe
utafute njia ya kwenda,” alisema huku akishangiliwa.
Akifafanua zaidi,
Waziri Mkuu alisema vita inayoendeshwa imelenga kuifanya Tanzania
ibadilike na itoke kwenye uchumi wa chini na kuingia uchumi wa kati.
“Swali la msingi ni je tunafikaje hapo? Jibu ni kupitia uzalishaji wa
bidhaa viwandani,” alisema.
“Nyote ni mashahidi wa
jinsi ambavyo shilingi yetu imekuwa ikishuka thamani kulinganisha na
dola ya Marekani. Tulitoka sh. 1,600/-, tukapanda hadi sh. 1,900/- na
sasa tumefikia sh. 2,180/-. Hii ni kwa sababu tunaagiza zaidi bidhaa
kutoka nje ya nchi badala ya kuzalisha, hatuwezi kuendelea hivi na ndiyo
maana tumeamua kuwa nchi ya viwanda. Leteni mitaji nyumbani muwekeze,”
alisisitiza.
Akijibu swali kuhusu
Serikali kutafuta njia ya kutoa mikopo kwa Watanzania waishio nje ya
nchi, Waziri Mkuu alisema mkopo ni mkataba kati ya taasisi ya kifedha na
mkopaji kwa hiyo Serikali haiwezi kubeba dhamana hiyo. “Benki wanataka
ijue taarifa zako mkopaji, wanataka wajua dhamana zako ni zipi,
wajiridhishe na shughuli unazofanya. Je panakopesheka hapo?,” alihoji.
Hata hivyo, aliwaeleza
kwamba wakitaka kuwekeza nyumbani wanaweza kupata mikopo kutoka benki ya
maendeleo ya kilimo (TADB), Benki ya Rasilmali (TIB Corporate na TIB
Development). “Hizi benki ni za wakulima na wajasiriamali, na zina
masharti yake, kwa hiyo ni lazima wakakague eneo lako au mahali
unapofanyia biashara au wakague leseni yako na ukweli wa maombi
uliyopelekea. Sasa ukiwa Zambia watawezaje kukukopesha? Kwa hiyo ukitaka
fedha uwe nyumbani,” alisema.
Akijibu swali ni vipi
Serikali itawasaidia wanadiaspora kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu
wakiwa nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema Serikali haijawahi kujaribu
jambo hilo licha ya kuwa ilikwishapokea mapendekezo kadhaa kutoka nchi
mbalimbali lakini kwa vile wameliuliza, yeye analibeba na kwenda
kulifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment