Kivuko cha Magogoni kikiwa katika ukarabati katika Bandari ya Dar es Salaam.
Picha na Theresia Mwami-TEMESA.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imetembelea na kujionea maendeleo ya
ukarabati wa kivuko cha Mv Magogoni chini ya kampuni ya Songoro Marine
katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Herbert Mrango ameeleza kuridhishwa na
kasi ya ukarabati wa kivuko hicho na kuushauri uongozi wa TEMESA
kuharakisha malipo yanafanyika kwa wakati ili kukamilisha kazi hiyo
ndani ya muda uliopangwa.
“Nakuagiza Kaimu Mtendaji
uhakikishe malipo kwa kampuni hii yanafanywa kwa wakati na ukarabati huu
kukamilika mapema ili kuwapa fursa wananchi kutumia kivuko hiki”alisema
Balozi Mrango.
Aliongeza kuwa ni muhimu wananchi
kurejeshewa huduma ya kivuko hicho ili kuondoa kero inayowakabili kwa
sasa kwa kuwa na kivuko kimoja chenye uwezo wa kubeba magari ambapo
kukamilika kwa ukarabati wa huu utakuwa umerahisiha shughuli ya
usafirishaji.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji wa
TEMESA Mhandisi Manase Ole kujan amesema atahakikisha malipo
yanafanyika kwa wakati ili kuwezesha mkandarasi huyo kumaliza kazi hiyo
kwa muda uliopangwa na kurejesha huduma ya kivuko hicho kwa wananchi.
Aidha aliongeza kuwa kazi ya
ukarabati wa kivuko hicho imegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni,
ukarabati wa “Body” pamoja na mifumo ya umeme unaofanywa na Mkandarasi
kutoka kampuni ya Songoro Marine huku TEMESA ikihusika na ukarabati wa
mitambo ya kuongozea kivuko.
Kivuko cha Mv Magogoni
kinachotoa huduma katika maeneo ya kigamboni na Magogoni Jijini Dar es
Salaam kilisimamisha rasmi kutoa huduma hiyo mapema Mei mwaka huu kwa
ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa chini ya Wakala wa Ufundi na Umeme
(TEMESA) na kampuni ya Songoro Marine kukiongezea ufanisi katika kutoa
huduma ya usafiri kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment