Na Mwandishi wetu
Serikali imebainisha kuwa Sheria
Mpya ya Ushirika (Sheria namba 6 ya mwaka 2013) imesaidia kupunguza
changamoto za wanachama wa Vyama vya Ushirika pamoja na wakulima wa
Tumbaku nchini.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi Mhe. Tate William Ole-Nasha aliyasema hayo leo bungeni Mjini
Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge kwenye kipindi cha maswali na
majibu.
Mhe. Ole-Nasha alisema kuwa
baadhi ya marekebisho ya Sheria hiyo yanayowanufaisha wanachama wa Vyama
vya Ushirika wakiwemo wakulima wa tumbaku ni pamoja na kuwachukulia
hatua viongozi wabadhirifu wa vyama hivyo.
“ Katika maeneo yanayolima
tumbaku viongozi wabadhirifu wa Vyama vya Ushirika 26 Mkoani Ruvuma
wakiwemo Maafisa Ushirika wawili wamesimamishwa kazi na kufikishwa
mahakamani.” alisema Ole-Nasha.
Pia Mhe. Ole-Nasha alifafanua
kuwa sheria ya sasa inakataza vyama kukopa zaidi ya asilimia 30 ya mali
zake (Own Capital) ili kuzuia vyama hivyo kuingia kwenye madeni makubwa
yasiyolipika na hatimaye kusababisha migogoro ndani ya vyama.
Akizungumzia mafanikio upande wa
tozo, Ole-Nasha lisema kuwa kuanzia sasa Mkutano Mkuu utakuwa chini ya
uenyekiti huru utakaochaguliwa na wajumbe wa mkutano huo kinyume na
awali ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa
Mkutano Mkuu.
“Lengo ni kulinda maslahi ya
wakulima ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tozo zote zinazoidhinishwa
na Mkutano Mkuu zinakuwa na maslahi kwa wakulima wa Tumbaku.” Aliongeza
Ole-Nasha.
Kwa mujibu wa Ole-Nasha Serikali
inatambua uwepo wa kodi nyingi na tozo kwenye mazao mbalimbali ya
chakula na biashara hivyo kwa kushirikiana na wadau imedhamiria
kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika sekta ya kilimo kwa
kupitia upya taratibu, vibali, tozo, kodi, ushuru na ada nyingine
zinazotozwa ili kutoa nafuu kwa wakulima.
No comments:
Post a Comment