WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
anatarajiwa kuondoka nchini leo jioni (Jumanne, Mei 10, 2016) kwenda
London, Uingereza kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi unaojadili suala
la kupambana na rushwa (Anti-Corruption Summit 2016) utakaofanyika Mei
12, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo mchana, Waziri Mkuu alisema anaenda kumwakilisha Mheshimiwa Rais,
Dk. John Pombe Magufuli kwa sababu siku hiyo hiyo, atalazimika
kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri
Museveni.
“Mheshimiwa Dk. Magufuli ni
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na siku hiyo hiyo,
mmoja wa marais wa nchi wanachama anaapishwa. Kwa hiyo amelazimika
kwenda kuhudhuria sherehe hizo,” alifafanua Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu mada ya
mkutano huo, Waziri Mkuu amesema Tanzania inafanya vema katika mapambano
dhidi ya rushwa na kwamba baadhi ya nchi zimeanza kuvutiwa na juhudi
ambazo Serikali imekuwa ikichukua.
“Waziri Mkuu wa Uingereza ameandaa
mkutano huu na alimwalika Mheshimiwa Rais Magufuli ili ahudhurie akiwa
ni miongoni wa wakuu wa nchi 60 watakaohudhuria mkutano huo. Tanzania ni
miongini mwa nchi mbili kutoka bara la Afrika ambazo zimealikwa
kushiriki. Nchi nyingine ya kutoka Afrika ni Nigeria,” alisema.
Waziri Mkuu atafuatana na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Kimataifa na Kikanda, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Mkurugenzi wa
TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola, wataalamu wa sekta ya rushwa na
wanasheria
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 10, 2016.
No comments:
Post a Comment