SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar
imewataka Wazazi, Walezi na Wazee kuwalinda watoto wao dhidi ya
Mazingira hatari yanayowazunguka ili kuwaepusha na athari za vifo pamoja
na ulemavu.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa
Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar, Mauldine Castiko wakati
akiwafariji wahanga wa tukio la vifo vya watoto wawili waliotumbukia
katika Kisima cha Maji na kupoteza maisha huko katika mitaa ya Tomondo
Uzi, Unguja.
Alisema wazazi na jamii kwa
ujumla wanatakiwa kuwa waangalifu katika mazingira wanayoishi kwa
kuyaweka katika hali ya usalama ili kuwaepusha na madhara watoto wadogo
yanayoweza kuwasababishia vifo na hatari zingine zinazoepukika.
Castiko alitoa mkono wa pole kwa
familia hiyo na kuwaomba waendelee kuwa wavumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba wa watoto hao wasiokuwa na hatia.
Aliisihi familia hiyo kuendelea
kuvumilia katika kipindi kigumu cha msiba huku watu waliohusika na
uzembe wa kusababisha vifo vya watoto hao wachukue juhudi za haraka kwa
kufunika Kisima hicho ili kisiendelee kuhatarisha maisha ya watoto
wengine mtaani.
Alisema serikali imesikitishwa na
tukio hilo la vifo vya watoto wasiokuwa na hatia na kuahidi kutoa
ushirikiano wa hali na mali kwa familia hiyo.
Alizitaka mamlaka zinazohusika na
masuala ya ulinzi wa Raia na Mali zao kuendelea kufanya uchunguzi wa
kina juu ya tukio hilo ili watu watakaobainika kuhusika kwa uzembe na
tukio wachukuliwe hatua za kisheria.
“Familia, Ndugu na Jamaa wa marehemu nakupeni pole na kukuombeni muendelee kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Lakini pia nachukua fursa hii
kuwaomba wazazi na walezi kuwa makini na watoto wenu hasa awa wadogo
kwani mazingira wanayokuwa wakicheza mengi hayana usalama juu ya maisha
yao.”, alisisitiza Waziri huyo na kuongeza kuwa serikali haitowavumilia
watu wanaohatarisha maisha ya watoto kwa makusudi na hatakayebainika
akifanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Waziri huyo alifafanua kwamba
Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 pamoja na Mikataba mbali mbali ya
Kimataifa inayohusika na Haki za Binadamu iliyoridhiwa na serikali ya
Tanzania inatambua na kutetea haki za Watoto kuhakikisha wanapata ulinzi
wa kuishi na huduma mbali mbali za msingi kama walivyo watu wengine.
Alisema Serikali ya mapinduzi ya
Zanzibar inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuhakikisha maisha ya
watoto yanakuwa salama wakati wote wakiwa ndani na nje ya familia zao
huku ikiimarisha sheria na miongozo ya kusimamia haki zao Kikatiba.
Alitoa agizo kwa wananchi wote wa
Zanzibar wanaomiliki visima vya maji ama kuchimba mashimo mbali mbali
yanayoweza kuhatarisha maisha ya watoto, kufukia ama kuvifunika
visihatarishe maisha ya watoto wengine.
Aidha alisema jamii inatakiwa
kuwa makini na watoto wadogo hasa kwa kipindi hiki cha maradhi ya
miripuko ya Kipindupindu kwa kuwaepusha watoto wasile wala kunywa maji
machafu na vyakula visivyokuwa salama kwa afya zao.
“ Kuna baadhi ya familia
hawafutilii mwenendo wa watoto wao pindi wanapokuwa nje ya majumba yao
kujua wanakula nini wala wanacheza katika mazingira gani hali ambayo
inaweza kuwaweka katika mazingira hatarishi watoto wetu.”, alisema
Waziri huyo.
Naye Mama mzazi wa watoto hao,
Mariam Hassan alishukuru ujio wa kiongozi huyo na kueleza kwamba vifo
vya watoto hao ni pigo kubwa kwa familia yake.
Alisema kwamba watoto hao
walikuwa mazingira ya mtaani wakicheza ambapo yeye alikuwa akiendelea na
harakati za kuandaa chakula cha mchana ghafla majira ya saa 7:30 mchana
akaambiwa kwamba watoto wake wamedondoka katika kisima cha jirani yao
hapo mtaani.
Baada ya kupata taarifa hiyo
alifika katika kisima hicho ambapo alikuwa watu mbali mbali wakiendelea
na juhudi za kuokoa maisha ya watoto hao lakini walipotolewa walikutwa
washafariki kwani haikujulikana wameingia wakati gani.
Aliwataja watoto hao kuwa ni
Yussuf Faki Juma mwenye umri wa miaka miwili(2) na Muhamadi Ali Abdallah
umri wa mwaka 1 na miezi nane wote wakiwa watoto wa familia moja.
No comments:
Post a Comment