(TAARIFA KWA UMMA)
TAARIAFA YA WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU
YA KIMATAIFA YA FAMILIA INAYOADHIMISHWA TAREHE 15 MEI, 2016
Tarehe 15 Mei ya kila mwaka,
Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa
kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia. Maadhimisho haya yametokana na
Tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/257 la tarehe 20 Septemba,
1993, linalohimiza nchi wanachama kuwa na siku maalum ya Familia.
Lengo la Maadhimisho haya ni
kutambua umuhimu wa familia kama kitovu cha Maendeleo katika jamii na
pia kuzienzi familia kwa kuzipa siku maalum ya maadhimisho kuwezesha
kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. Aidha, kutambua kuwa
uzingatiaji wa masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi hupaswa
kujadiliwa, kupangwa na kutekelezwa kuanzia ngazi ya familia kwa ajili
ya kuimarisha ushiriki thabiti wa jamii katika maendeleo ya taifa lao.
Mwaka 2016, Tanzania itaadhimisha siku hii katika ngazi ya mikoa na
wilaya kulingana na taratibu na mazingira ya mikoa husika. Maendeleo ya
nchi hayawezi kufikiwa kama familia hazitakuwa na afya bora. Kwa
kutambua hili, Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia
2016 inasema: “Familia Yenye Afya Bora ni Mwanga wa Maendeleo”.
Kauli
mbiu hii inalenga kuchochea mafanikio ya malengo ya Maendeleo Endelevu
yatakayozingatia uboreshaji wa huduma ya afya bora ya familia zetu, kuwa
na malezi bora ya watoto na kusisitiza utunzaji wa afya ya wanajamii
wenye mahitaji maalum wakiwemo wazee na watu wenye ulemavu. Wizara
inatoa wito kwa kila mwanafamilia kushiriki maadhimisho ya Siku hii
muhimu kwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Aidha, tunaomba
vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Maadhimisho
haya ili kuharakisha uboreshaji wa afya za wanafamilia wote katika nchi
yetu.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
No comments:
Post a Comment