Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya
nishati, Dk. Juliana Pallangyo (pichani) akisoma hotuba ya ufunguzi wa
mkutano wa siku tatu jijini Dar es Salaam uliokutanisha wataalam
kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujadili taarifa ya mtaalam
mwelekezi kuhusu utafiti uliofanywa katika Ziwa Ngozi lililopo mkoani
Mbeya ambapo kuna viashiria vya jotoardhi pamoja na eneo la Kibiro
nchini Uganda.
Wataalam
mbalimbali wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya
nishati, Dk. Juliana Pallangyo ( anayeonekana mbele kwa mbali)
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya
nishati, Dk. Juliana Pallangyo (wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele)
akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo mara baada ya
ufunguzi.
Na Tabu Mullah
Imeelezwa kuwa Tanzania inatarajia
kuzalisha megawati 100 ndani ya kipindi cha miaka saba ijayo na
kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es
Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo katika
mkutano uliokutanisha wataalam kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya
kujadili taarifa ya mtaalam mwelekezi kuhusu utafiti uliofanywa katika
Ziwa Ngozi lililopo mkoani Mbeya ambapo kuna viashiria vya jotoardhi
pamoja na eneo la Kibiro nchini Uganda.
Wataalam katika mkutano huo
ulioandaliwa na Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC)
kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje Iceland, wanatoka katika
nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Marekani,
New Zealand na Djibouti.
Akizungumza katika ufunguzi wa
mkutano huo wa siku tatu Dk. Pallangyo alisema kuwa kutokana na
ugunduzi wa nishati ya jotoardhi nchini Tanzania, serikali imeweka
mikakati ya kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka saba ijayo
inazalisha megawati 100 zitakazoongezwa kwenye gridi ya taifa na
hivyo kupunguza tatizo la upungufu wa umeme nchini.
Alisema kuwa serikali imeweka
mkakati wa kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inachangia katika ukuaji
wa uchumi na kupelekea nchi kutoka kwenye orodha ya nchi masikini
duniani na kuingia katika nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025,
kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyofafanua.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa nishati
ya uhakika kutavutia uwekezaji kwenye viwanda na kuzalisha ajira na
nchi kupiga hatua kimaendeleo.
Alisisitiza kuwa Tanzania ina
nishati ya kutosha ya jotoardhi yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa
megawati 5000 ambayo haijatumika bado ambapo serikali imeweka mikakati
mbalimbali ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kampuni ya Maendeleo ya
Jotoardhi Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO).
Aliendelea kusema kuwa TGDC
ilianzishwa Desemba 2013 kwa madhumuni ya kusimamia maendeleo ya
jotoardhi nchini Tanzania na kuanza rasmi shughuli zake Julai 2014
jukumu lake kuu likiwa ni kutafiti, kuchimba na kutumia rasilimali za
jotoardhi kwa uzalishaji umeme na matumizi mengine ya moja kwa moja.
No comments:
Post a Comment